Monday, 13 July 2026

MUHTASARI WA KIKAO CHA WANAUKOO WA MALINGO CHA 28.06.2026

MUHTASARI WA KIKAO CHA WANA UKOO WA MALINGO KILICHOKETI TAREHE 28/06/2026 KWENYE MJI WA MAREHEMU MZEE METHUSELA KAJANA MALINGO. WAJUMBE: Kikao kilihudhuriwa na Wajumbe wapatao 30. Kilisimamiwa na Bigambo Aman aliyekuwa M/kiti, Dishon Kajana Malingo aliyekuwa Katibu na Seleman Ediga Kajana aliyekuwa mweka kumbukumbu wa Kikao (Mwandishi). AGENDA: 1. KUFUNGUA KIKAO Kikao kilifunguliwa na M/kiti wa kikao ndugu Bigambo Aman mnamo saa 3:25 alasiri. M/kiti aliwashukuru wajumbe kwa kutoa muda wao na kuhudhuria kikao. Kabla ya kuanza kikao, ombi la kukiweka kikao uweponi mwa Bwana lililetwa na Mke wa Marehemu Methusela Kajana Malingo Bi Mariam Matama. 2. UTAMBULISHO Baada ya kikao kufunguliwa mwenyekiti alifanya utambulisho wa wajumbe wote waliokuwepo kwenye kikao. Zoezi hili la utambulisho lilisaidia wajumbe kufahamiana kwa kina. 3. KUSOMWA KWA MUHTASARI WA KIKAO KILICHOPITA Muhtasari wa kikao kilichopita cha tarehe 26/02/2025 ulisomwa na Katibu wa Vikao vya Ukoo wa Malingo Ndugu DISHON KAJANA MALINGO. Kupitia muhtasari huu, wajumbe waliweza kufahamu kwa kina kile kilichoazimiwa kwenye kikao husika. Aidha tathmini ya yale yaliyohitaji utekelezaji ilifanyika. 4. MABADILIKO YA TAREHE YA KUFANYIKA KWA VIKAO VYA UKOO WA MALINGO Kutokana na kuwepo kwa changamoto kwa tarehe iliyokuwa imependekezwa hapo awali yaani 30/7 kila mwaka, kikao kiliazimia kufanya mabadiliko na kupendekeza tarehe 28/6 kila mwaka kuwa tarehe ya kufanyika kwa vikao vya ukoo wa Malingo kila mwaka. 5. KUWEKA ALAMA KWENYE MIPAKA PAMOJA NA URASIMISHAJI WA ARDHI YA UKOO Kikao kiliazimia kuwa ili kuondoa migogoro kati ya ardhi ya uzao wa Maingu Malingo na Kajana Malingo, ziwekwe alama zikazokuwa utambulisho wa kudumu kati vizazi vya sasa na vijavyo. Sanjari na hilo, kikao pia kiliazimia kurasimisha ardhi hii na kupata hati miliki yake ili kuondoa mgogoro kati ya wana ukoo na serikali. Jukumu la kurasimisha ardhi hii lilikasimishwa kwa Judith Kajana Malingo ili afuatilie michakato yote husika. 6. UDUMISHAJI WA MAADILI NDANI YA UKOO Kikao kilibaini uwepo wa wana ukoo ambao wamefikisha umri wa kuoa na hawajaoa kwa sababu zao zisizo na msingi wowote. Hili linaonesha kushuka kwa maadili ndani ya ukoo. Kwa hoja hii, kikao kilitoa azimio kuwa kwa wana ukoo wote walio katika ukapera usio na sababu zozote wanatakiwa kuwa wameoa mara tutakapo kutana kwenye kikao kijacho cha tarehe 28/06/2027 kama tukijaliwa uzima. 7. KUDUMISHA UDUGU NA USHIRIKIANO NDANI YA UKOO. Ili kudumisha mshikamano na udugu ndani ya ukoo, kikao kiliazimia kuwa wana ukoo wote hawana budi kujumuika kwa pamoja katika matukio mbalimbali ya kijamii ikiwepo misiba na sherehe. Aidha kujuliana hali kwa wanandugu ni suala muhimu katika kudumisha udugu hivyo halina budi kufanyika mara kwa mara. 8. UJENZI WA KABURI LA MASIGE MALINGO Kutokana na kaburi hili kuwa katika hali mbaya, kikao kiliazimia kwa pamoja kufanyika kwa ujenzi wa dharura ili kulinusuru lisiharibike na hatimaye kupotea kabisa. Wana ukoo walikubaliana kila mwana ukoo kutoa mchango ili kukamilsha ujenzi wa kaburi hili linalogharimu kiasi cha Tsh 300,000/=. Ujenzi unatarajiwa kufanyika haraka iwezekanavyo ndani ya mwezi Agosti mwaka 2026. 9. HOJA YA KUIMARISHA UCHUMI MIONGONI MWA WANA UKOO. Imebainika kuwa wana ukoo walio wengi hawana shughuli za kuwaingizia kipato hali inayozorotesha uchangiaji katika matukio mbalimbali ndani ya ukoo. Kutokana na hali hii, kikao kiliazimia kwa kutoa ushauri kwa kila mwana ukoo kutafuta shughuli ya kufanya ili kujiimarisha kiuchumi. Aidha kikao kilitoa rai kwa wana ukoo kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kijamii ili kupata msaada wa kijamii pale wanapopatwa na matatizo mbalimbali. Hili lilienda sambamba na kuwahimiza wana ukoo wote wanaoishi mikoa mbalimbali nchini kujiunga na Nzengo ili kutambulika na kupata msada wa haraka pale wanapopata matatizo mbalimbali hususani misiba. 10. MENGINEYO. Katika hoja hii ya mengineyo, mambo kadhaa yalibainishwa na wana ukoo kama ifuatavyo: a) Kuna wana ukoo ambao watoto wao hawafahamiki kwa wana ukoo. Kutokana na kuwepo kwa jambo hili, kikao kilitoa rai kwa wana ukoo kutambulisha watoto wao kwa kuwaleta nyumbani kwenye chimbuko lao hili wana ukoo waweze kuwafahamu. b) Kuna baadhi ya makaburi ya wana ukoo hayafahamiki yalipo. Kikao kiliazimia kuwa makaburi hayo yatafutwe na yabainishwe yalipo ili taratibu zingine za kuyaweka katika hali nzuri ziweze kufanyika. Mfano ni kaburi la Bibi Nyamarwa ambaye ni mke wa Mzee Malingo Melijo halifahamiki lilipo. c) Kikao kijacho kilipangwa kufanyika Siku ya Jumatatu tarehe 28/6/2027 kwenye mji wa marehemu Mzee Methusela Kajana Malingo. Aidha michango ya ufanikishaji wa kikao hicho unatakiwa kukamilika mwezi mmoja kabla ya tarehe ya kikao. 11. KUFUNGA KIKAO Baada ya kikao kuhitimisha agenda zake, mwenyekiti ndugu Bigambo Amani aliwashukuru wajumbe kwa michango yao chanya na uvumilivu wao waliouonesha tangu kuanza kwa kikao mpaka muda wa kuhitimisha. Aidha mjumbe yule yule aliyeleta ombi la ufunguzi alitoa ombi kwa mara nyingine akimshukuru Mungu kwa namna alivyokiongoza kikao kufanyika katika hali ya utulivu. Baada ya sala hiyo mwenyekiti alihitimisha kikao yapata saa 6:40 jioni kwa kuwasihi wajumbe kuonesha mwitikio huo huo katika kikao kijacho mwezi Juni 2027. Muhtasari huu umeandaliwa na ndugu Seleman Ediga Kajana (Mweka kumbukumbu) Leo Tarehe 28/06/2026.

Labels: ,

0 Comments:

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home