Saturday, 24 November 2018

Daktari na Mwalimu


Daktari na Mwalimu

Daktari
Hii kazi ya Mwalimu, kweli haina thamani,
Ni kama mwendawazimu, kelele kutwa shuleni,
Na mimi siheshimu, sitii maanani,
Kazi ya kujivunia, kweli ni ya Daktari.


Mwalimu
Ni wewe mwendawazimu, huna akili kichwani,
Wasema bila fahamu, hujui wasema nini,
Udokta hautimu, bila kufika shuleni,
Kazi njema ya walimu, kutoa watu gizani.

Daktari
Kusoma hailazimu, mtu afike shuleni,
Kuna wengi mumu humu, wasomea barazani,
Na mengi wayafahamu, yaliyomo vitabuni,
Daktari ni muhimu, kwa kuokoa maisha.

Mwalimu
Hilo si maalumu, kuokoa maishani,
Tena unajidhulumu, waingia kufuruni,
Hiyo kazi ya Karimu, ndiye mwenye nusurani,
Kazi njema ya walimu, kutoa watu gizani.
Daktari
Daktari ni muhimu, kukutoa ujingani,
Mtu amekula sumu, maisha ya hatarini,
Budi atajilazimu, afike kwangu nyumbani,
Daktari ni muhimu, kwa kuokoa maisha.
Mwalimu
Asili ya binadamu, yatokana na manani,
Narudi kutakalamu, nililosema mwanzoni,
Asipopenda Karimu, bidiizo zifaeni?
Kazi njema ya walimu, kutoa watu gizani.
Daktari
Hilo nalifahamu, silipingi abadani,
Amri ni ya Karimu, najua toka zamani,
Japo mtu hana damu, asubiri kwa Manani,
Daktari ni muhimu, kwa kuokoa maisha.
Mwalimu
Kidogo natabasamu, na kicheko mdomoni,
Wa tele wendawazimu, moja ni wewe fulani,
Hivyo wale marehemu, hawakwenda ugangani?
Kazi njema ya walimu, kutoa watu gizani.
Daktari
Hilo mimi sikubali, nitafanya nushindani,
Bora kuomba Jalali, si lazima ugangani.
Unapopata ajali, mbona hukai nyumbani?
Daktari ni muhimu, kwa kuokoa maisha.
Mwalimu
Hayo yako sikubali, na wala siyaamini,
Tokea enzi azali, hako Daktari nchini,
Watu hupata thakili, hutibiwa majumbani,
Kazi njema ya walimu, kutoa watu giza

Labels:

1 Comments:

At 21 July 2022 at 18:40 , Anonymous Anonymous said...

victor

 

Post a Comment

Subscribe to Post Comments [Atom]

<< Home