Ripoti ya utafiti kuhusu sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo walio nao katika kufundisha na athari zake katika kutoa elimu bora
Thursday, October 20, 2011

Je, Walimu wetu wana Sifa za Ualimu na Hamasa ya
Kufundisha?
Ripoti ya utafiti kuhusu sifa za waalimu kitaaluma,
hamasa na moyo walio nao katika kufundisha na athari zake katika kutoa elimu
bora
Oktoba 2011
Shukrani
Utafiti huu ni jitihada za pamoja kati ya HakiElimu
na Idara ya Saikolojia ya Elimu na Mafu
nzo ya Mitaala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa
ushirikiano na Wafanyakazi wa HakiElimu Dk. Kitila Mkumbo
aliandaa mpango na tafiti pendekezo na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu
njia za ukusanyaji wa taarifa. Pia alisimamia mchakato mzima wa utafiti na
kuandika ripoti kuu.
Wafanyakazi wafuatao walifanya kazi ya utafiti kwa
kutembelea maeneo ya utafit
engo la kukusanya data: Elizabeth Missokia, Daniel Luhamo, Charles Mtoi, Robert Mihayo, Glory Mosha, Fausta Musokwa, Naomi Mwakilembe, Edwin Mashasi, Benedicta Mrema, Boniventura Godfrey, Lilyan Omary, Anastazia Rugaba, Frederick Rwehumbiza, Nyanda Shuli, Vicent Mnyanyika na Esther Mashoto.i kwa l
Ripoti hii iliandikwa na Dk. Kitila Mkumbo. Uhariri,
tathmini pamoja na ushauri kuhusu ripoti ulitolewa na Elizabeth Missokia, Mtemi
Gervas Zombwe, Robert Mihayo na Nyanda Shuli.
Ripoti ya utafiti huu isingefanikiwa bila ya ushirikiano
wa wanafunzi, wazazi, wajumbe wa kamati za shule, walimu pamoja na wafanyakazi
katika ofisi za wilaya ambao tulifanya nao mahojiano. Tunawashukuru sana
kwa michango yao pamoja na utayari wao kufanya kazi nasi.
© HakiElimu 2011,
ISBN: 978-9987-18-019-6
HakiElimu, S.L. P 79401, Dar es Salaam, Tanzania
Simu: (255 22) 2151852/3, Faksi: (255 22) 2152449
Sehemu yoyote ya ripoti hii inaweza kunukuliwa kwa ajili
ya matumizi ya elimu na si ya kibiashara, ili mradi tu chanzo kitatajwa na
kwamba nakala mbili zitatumwa HakiElimu.
Yaliyomo
Marejeo39
Majedwali
Usuli wa hitaji
la kufanya utafiti
Utoaji wa elimu bora ni jambo muhimu katika kuchochea
maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa hakika, waandishi wengi wanaona kuwa
elimu bora ndiyo njia yenye ufanisi zaidi katika kujenga maadili, mitazamo,
tabia na maarifa muhimu kwa watu binafsi ili waweze kutumika kwa manufaa katika
jamii iliyotangamana. Kikao cha tatu cha Mkutano Mkuu wa 61 wa Umoja wa Mataifa
(GA/SHC/3847) kilisisitiza umuhimu wa elimu bora katika kuleta maendeleo ya
jamii, kikitaja kwamba elimu bora ni jambo muhimu sana katika kuleta demokrasia
ya kweli na ajira ya kweli. Hali kadhalika, Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025)
inataja kwamba elimu bora ni muhimu ikiwa taifa litakubali kikamilifu kupambana
na changamoto za maendeleo zinazolikabili.
Kuna viashiria kadhaa vya elimu bora. Viashiria viwili
kati ya hivyo ni muhimu sana, navyo hutumiwa mara kwa mara katika nchi nyingi.
Kiashiria cha kwanza huangalia utendaji wa wanafunzi katika maarifa ya msingi,
ambayo ni kusoma, kuandika na kuhesabu. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni
(Uwezo, 2010) inaonyesha kuwa, ingawa kumekuwa na mafanikio makubwa katika
kuandikisha watoto shule, kujenga shule na kutoa mafunzo kwa waalimu, wanafunzi
hujifunza maarifa machache mno nchini Tanzania; kiasi kwamba pindi wanapohitimu
elimu ya msingi, wanafunzi huwa hawana maarifa ya msingi ya kusoma, kuandika na
kuhesabu. Na kiashiria cha pili huangalia matokeo ya mitihani ya taifa.
Nchini Tanzania, mitihani hii ya taifa ni ile
inayoandaliwa na kusimamiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania. Mitihani ya
taifa ni mojawapo ya viashiria vyenye nguvu kuhusu kiwango cha elimu, navyo
hutumiwa kufanya maamuzi yahusuyo watu binafsi na taasisi kupitia matokeo ya
mitihani. Mitihani ni kiashiria muhimu pia cha kupima watoto wamejifunza kiasi
gani, nayo ni chanzo muhimu cha taarifa kwa wazazi pindi wanapofanya maamuzi
kuhusu watoto wao. Kwa kutumia kipimo hiki, tunaweza kutoa maoni kwamba kiwango
chetu cha elimu kimekuwa kikiporomoka katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita.
Mathalani, kama Kielelezo 1 kinavyoonyesha, Matokeo ya Mtihani wa Taifa
wa Kidato cha Nne Mwaka 2010 yalitikisa nchi nzima baada ya wanafunzi wengi
kufeli. Kati ya watahiniwa 354,042 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha
Nne Mwaka 2010, watahiniwa 177,021 (sawa na 50%) walipata Daraja la Sifuri, nao
watahiniwa 136,633 (38.6%) walipata Daraja la Nne. Watahiniwa 15,335 (4.3%)
pekee ndio waliopata Daraja la Kwanza na la Pili, ilihali asilimia 88.6 ya
watahiniwa walipata Daraja la Nne na Daraja la Sifuri!
Hivyo basi, kusema kweli, asilimia 88.6 ya watahiniwa walifeli Mtihani
wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010 kwani hawawezi kuendelea na elimu ya
ngazi yoyote ya juu. Athari za kufeli huku ni kubwa mno. Itawawia vigumu mno
wanafunzi hawa waliofeli kupata ajira kwani hawana maarifa ya msingi ya kusoma,
kuandika na kuhesabu. Pia wanakosa stadi za msingi za maisha kama kujiamini,
ubunifu na mbinu za kutatua matatizo.
Sababu kadhaa zimetajwa kuwa chanzo cha hali duni ya
elimu hapa nchini. Mosha (2011) ameeleza kwa muhtasari sababu hizo, akiziweka
katika makundi makuu mawili, ambayo ni: sababu za kimazingira na sababu za
vitendea kazi. Kwa mujibu wa Mosha, sababu za kimazingira hujumuisha mazingira
ya kisiasa, kiuchumi, kisheria, kidemografia, kiutamaduni na kimataifa. Sababu
za vitendea kazi hujumuisha uongozi duni katika taasisi, ufadhili duni kwa
sekta ya elimu, hali duni ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, walimu
wenye sifa duni na matatizo ya mitaala. Elimu bora imehusishwa pia na utoaji na ustadi wa
waalimu (Oduro, Dachi & Fertig, 2008). Oduro na wenzie wamedai kuwa
mabadiliko katika elimu barani Afrika yamelenga zaidi kuongeza idadi ya watu
wanaopata elimu, huku ubora wa elimu inayotolewa ukipewa umakini mdogo.
Sababu nyingi za kuwepo kwa hali duni ya elimu
zilizobainishwa na tafiti zilizotangulia zimekuwa zikizungumzia zaidi kuwepo
kwa miundombinu isiyofaa ya kufundishia na kujifunzia. Hususan, kumekuwa na
tafiti chache sana ambazo zimelenga kuzungumzia ubora wa waalimu na moyo wao wa
kujitolea kama mambo yanayoukilia ujifunzaji wenye ufanisi ambao hatimaye
huleta mafanikio kitaaluma. Hakika, uchunguzi wa kina wa programu mbalimbali za
zamani na za sasa za kuleta mabadiliko katika elimu zilizoasisiwa na Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi unaonyesha, miongoni mwa mambo mengine, kuwepo kwa
msisitizo mdogo sana kwa waalimu kama sehemu muhimu katika kuleta mabadiliko
katika mfumo wa elimu, hususan linapokuja suala la kuboresha ustawi wao na
weledi wao. Kwa mfano, kati ya maeneo 39 ya programu zilizopewa kipaumbele
katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), ni programu
mbili tu zinazogusia kwa mbali suala la kuboresha ustawi na weledi wa walimu.
Walimu ni sehemu muhimu katika kuleta elimu bora.
Elimu bora inahusiana moja kwa moja na ufundishaji bora na ujifunzaji bora.
Kuna mambo mengi yanayoukilia ufundishaji bora,miongoni mwayo ni sifa na uzoefu
wa waalimu, kiwango cha hamasa waliyo nayo, moyo wa kujituma na hisia za
kufundisha na mazingira ya kazi. Tafiti zinaonesha kuwa pindi waalimu
wanapokuwa na hamasa na wenye kuipenda kazi ya ualimu, wanafunzi huwa na hamasa
ya kujifunza na hujifunza maarifa yanayofundishwa na waalimu wao kwa ufanisi
zaidi (Caprara na wenzie, 2006). Hivyo basi, ni muhimu kuwatia hamasa waalimu
kama hatua mojawapo ya kushughulikia tatizo la kushuka kwa ubora wa elimu. Kwa
sababu hiyo, utafiti huu ulifanywa, kwa upande mmoja, kama hatua ya kujaribu
kuondoa pengo hili katika maarifa, na kwa upande mwingine, kuchunguza kwa
utaratibu maalumu hatua na mikakati ya kuongeza hamasa na moyo wa kujitolea wa
waalimu katika kufundisha.
Utafiti huu ulilenga kuchunguza jinsi sifa za waalimu kitaaluma na moyo
wao wa kujitolea katika kufundisha vinavyoathiri ubora wa elimu kama
unavyopimwa kwa kutumia ufaulu wa wanafunzi kitaaluma. Utafiti huu ulilenga zaidi:
· Kutathmini sifa za waalimu kitaaluma katika shule za sekondari za
serikali, binafsi na za jamii(kata) na jinsi zinavyohusiana na ufaulu wa
wanafunzi kitaaluma
· Kuchunguza utayari na moyo wa kujitolea wa waalimu katika kufundisha na
jinsi unavyohusiana na ufaulu wa wanafunzi kitaaluma
· Kubaini maoni ya wadau kuhusu kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika
mitihani ya taifa
· Kuchunguza vigezo vinavyotumiwa kuwapangia waalimu masomo ya kufundisha
na hamasa na moyo walio nao wa kufundisha masomo hayo
· Kuonyesha maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu namna ya kuboresha elimu
nchini Tanzania.
Ripoti hii inaonesha matokeo ya utafiti unaozungumziwa
hapa. Ripoti hii ina sehemu kuu nne, nazo ni usuli wa hitaji la utafiti, mbinu
za utafiti, matokeo ya utafiti, muhtasari, hitimisho na mapendekezo.
Sehemu ya Pili
Methodolojia
ya Utafiti
Utafiti huu ulishughulikia vipengele kadhaa vya ubora
wa elimu. Kwanza, utafiti ulitathimini sifa za walimu kitaaluma katika shule za
aina tatu, yaani shule za sekondari za serikali, shule za binafsi na shule za
jamii (kata). Pili, utafiti ulichunguza moyo wa kujitolea walio nao waalimu na
kuridhika kwao na kazi ya ualimu na jinsi mambo haya yanavyohusiana na ufaulu
wa wanafunzi. Kujituma na moyo wa kujitolea wa waalimu ulipimwa kwa kutumia
hojaji iliyofanyiwa marekebisho kutokana na zana ambazo zimekuwa zikitumiwa na
kuthibitishwa kimataifa, na vilevile kuwashirikisha waalimu katika majadiliano
ya vikundi lengwa (imeelezwa chini). Tatu, utafiti ulikusanya kwa mapana maoni
ya waalimu kuhusu namna ya kuboresha elimu mashuleni.
Hivyo basi, ni wazi kuwa utafiti huu ulichunguza suala
la ubora wa elimu kwa kutumia mitazamo ya waalimu. Utafiti huu ulitumia mbinu
mseto na vyanzo mbalimbali vya ukusanyaji data ambazo zilikuwa na msingi wake
katika mkabala wa kiidadi na mkabala wa kiubora. Mkabala wa kiidadi ulitumiwa
katika kukusanya taarifa za msingi za kiidadi kuhusu demografia ya walimu
na alama walizopata kuhusu mitazamo na moyo wa kujitolea walio nao. Mkabala wa
kuangalia ubora ulitumiwa kukusanya maoni ya walimu kuhusu kazi ya ualimu, na
vilevile maoni yao kuhusu hatua na mikakati ya kuboresha elimu nchini.
Utafiti huu ulifanywa katika mikoa sita, ambayo ni
Pwani, Mbeya, Kigoma, Singida, Dodoma na Mtwara. Mikoa hii ilichaguliwa kwa
makusudi kwa kuzingatia ufaulu wake katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne
Mwaka 2010, ambapo mikoa miwili ilichaguliwa kutoka kwenye makundi ya mikoa
iliyokuwa na ufaulu wa kiwango cha juu, kiwango cha kati, na kiwango cha chini.
Mikoa ya Pwani na Mbeya ilikuwa na ufaulu wa kiwango cha juu zaidi, ilhali
mikoa ya Kigoma na Singida ilikuwa na ufaulu wa kiwango cha kati, nayo Dodoma
na Mtwara ni mikoa iliyokuwa na ufaulu wa kiwango cha chini zaidi.
Katika kila mkoa, shule sita zilichaguliwa kwa
makusudi kushiriki katika utafiti huu. Kati ya shule hizi, mbili zilikuwa ni
shule kongwe za serikali, ambazo ziliitwa ‘shule za kitaifa za serikali’, mbili
zilikuwa ni shule za binafsi na mbili zilikuwa ni shule za jamii, ambazo
ziliitwa ‘shule za kata za serikali’. Shule zilichaguliwa kwa kutumia kigezo
cha ufaulu wake iwapo ni wa juu au chini na iwapo mahali ilipo shule ni mjini
au kijijini.
Kwa faida ya utafiti huu, ‘shule za kitaifa za
serikali’ zilitafsiriwa kuwa ni zile shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na
serikali ambazo zilianzishwa kuanzia wakati wa uhuru hadi mwaka 2000, kabla ya
kuanzishwa kwa programu maalumu ya serikali ya kujenga shule katika kila kata.
‘Shule za kata za serikali’ zinatafsiriwa kuwa ni shule ambazo zimejengwa na
wanajamii katika ngazi ya kata kwa msaada wa serikali, ambazo zinamilikiwa na
serikali. Hizi ni shule ambazo zimeanzishwa katika miaka ya 2000 kama sehemu ya
juhudi za serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya
sekondari.
Sampuli ya utafiti ilihusisha zaidi walimu na wakuu wa
shule. Walimu walishiriki kwa kujaza hojaji na kushiriki katika
usaili/majadiliano ya vikundi lengwa (taarifa zaidi zimetolewa katika kipengele
kinachofuata). Sampuli ya waalimu iliteuliwa kwa namna ifaayo kwani waalimu
wote waliohudhuria shuleni siku ambayo shule husika ilitembelewa ndio waliombwa
kujaza hojaji. Aidha, kati ya walimu sita hadi wanane katika kila shule
waliombwa kushiriki katika majadiliano ya kikundi. Hali kadhalika, wakuu wote
wa shule na Maafisa elimu wa wilaya zilizoshiriki walisailiwa.
Zana kuu nne zilitumiwa kukusanya data katika utafiti
huu. Kwanza, hojaji ziligawiwa kwa waalimu. Hojaji ya waalimu ilitumiwa
kutathmini vipengele vikuu vitano, ambavyo ni: sifa za awali za walimu,
mazingira ya kazi, hamasa waliyo nayo waalimu na mitazamo yao kuhusu
ufundishaji, moyo wao wa kujitolea kufundisha, na ufanisi wa uongozi wa shule.
Pili, majadiliano ya vikundi lengwa na usaili
vilifanywa kwa waalimu na wakuu wa shule. Kwa kiasi kikubwa mambo haya
yalilenga kuchunguza sababu za kushuka kwa kiwango cha elimu na maoni na
mitazamo kuhusu ufanisi wa walimu na moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu.
Tatu, kulikuwa na mwongozo wa taarifa za shule. Zana
hii ilitumiwa kukusanya data za msingi kuhusu shule, ikijumuisha idadi ya
walimu na sifa zao kitaaluma, upatikanaji na ubora wa zana za kufundishia na
kujifunzia, na ufaulu wa shule katika mitihani ya taifa katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita.
Data za kiidadi kutoka katika hojaji na miongozo ya
taarifa za shule iliingizwa katika programu ya kompyuta ya SPSS Toleo la 17.0.
Kisha data hizo zilisafishwa na uchambuzi muafaka ulifanywa. Kwa kiasi kikubwa
uchambuzi ulihusisha takwimu za kiuelezaji, ingawa uchambuzi wa takwimu
unaofikia matokeo kwa kujua sababu zake ulifanywa pia kwa kiwango kidogo.
Usaili na majadiliano ya vikundi lengwa yalirekodiwa
neno kwa neno katika vinasa sauti. Usaili na mahojiano haya yalinakiliwa katika
maandishi kwa Kiswahili na kutafsiriwa kwa Kiingereza. Mijalada ya lugha zote
mbili, Kiswahili na Kiingereza, ilihifadhiwa katika kompyuta na katika diski
mwako (flash discs) kama nakala za kumbukumbu. Data za kiubora
zilichambuliwa kwa kufuata kiunzi cha uchambuzi wa kimaudhui, ambapo maudhui
yalibainishwa na kufafanuliwa kwa kutumia nukuu za washiriki.
Sehemu ya Tatu
Matokeo ya
utafiti
Matokeo ya utafiti huu yamewasilishwa katika sehemu
kuu nne. Katika sehemu ya kwanza kumewasilishwa matokeo ya utafiti kuhusu
miongozo ya taarifa za shule, ambayo yanajumuisha data muhimu kuhusu shule kama
vile taarifa kuhusu historia yake, idadi ya walimu na sifa zao kitaaluma, na
vilevile ufaulu wa shule katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010.
Aidha, katika sehemu hii kumewasilishwa uhusiano uliopo kati ya sifa za waalimu
kitaaluma na ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo wa taifa. Katika sehemu ya
pili kumewasilishwa matokeo kuhusu hamasa waliyo nayo walimu na moyo wao wa
kujitolea katika kufundisha. Katika sehemu ya tatu kumewasilishwa matokeo
kuhusu mitazamo waliyo nayo walimu kuhusu kazi ya ualimu na hatua zipi
zichukuliwe kuboresha elimu nchini.
Kama ilivyoelezwa awali, jumla ya mikoa sita
ilifanyiwa utafiti. Katika kila mkoa, shule sita ziliingizwa katika sampuli ya
utafiti, na kufanya jumla yake kuwa shule 36 katika mikoa yote sita. Jumla ya
shule 30 zilishiriki kikamilifu katika utafiti (sawa na 83.3%). Hata hivyo,
shule 24 tu ndizo zilizojumuishwa katika uchambuzi wa mwisho. Shule zilizobaki
ziliondolewa kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba baadhi ya
shule hizo zilikuwa zikitoa elimu ya juu ya sekondari tu (kidato cha tano na
sita), ilhali kimsingi utafiti huu ulilenga shule zinazotoa elimu ya awali ya
sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne).
Kati ya shule hizo 24, kama Kielelezo 2
kinavyoonyesha, asilimia 29.2 zilikuwa shule za kitaifa za serikali, asilimia
37.5 zilikuwa shule za kata za serikali, asilimia 20.8 zilikuwa shule binafsi
zinazomilikiwa na asasi za Kikristo, asilimia 4.2 zilikuwa shule binafsi
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu na asilimia 8.3 zilikuwa shule binafsi
zinazomilikiwa na watu binafsi.
Idadi kubwa ya shule zilizotafitiwa zilianzishwa kati
ya mwaka 1990 na 2000 au baada ya mwaka 2000 (tazama Kielelezo 3). Kama
ilivyotarajiwa, na kama inavyooneshwa katika Kielelezo 4, idadi kubwa (85.7%)
ya shule za kitaifa za serikali zilizotafitiwa zilianzishwa kabla ya miaka ya
1990, wakati idadi kubwa (88.9%) ya shule za kata za serikali zilizotafitiwa
zilianzishwa baada ya mwaka 2000. Idadi kubwa (60%) ya shule binafsi
zinazomilikiwa na asasi za Kikristo na Kiislamu zilianzishwa kati ya mwaka 1990
na 2000, ilhali idadi kubwa ya shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za watu
binafsi zilianzishwa kabla ya mwaka 2000. Hii inaashiria kuwa, katika miaka ya
karibuni, serikali, kupitia juhudi mbalimbali za wanajamii, imekuwa mwanzilishi
mkuu wa shule za sekondari nchini.
Uchambuzi ulifanywa kuchunguza ufaulu wa wanafunzi
kitaaluma kwa kuzingatia umiliki wa shule. Ufaulu wa shule kitaaluma
ulichunguzwa kwa kuzingatia Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka
2010 ya shule husika. Matokeo hayo yameoneshwa kwa muhtasari katika Jedwali 1
na katika Kielelezo 5.
Pindi matokeo haya yalipochambuliwa kwa kuzingatia
kigezo cha umiliki, yalionyesha kuwa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za
Kikristo zilifaulu kwa kiwango cha juu sana kuliko zile zinazomilikiwa na asasi
nyingine. Kadhalika, kama ilivyotarajiwa, kwa ujumla, shule za kata za serikali
zilifanya vibaya sana katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne Mwaka 2010.
Mathalani, asilimia 65 ya watahiniwa katika shule za kata za serikali walipata
Daraja la Sifuri, huku asilimia 29.3 wakipata Daraja la Nne na asilimia 5.2 tu
wakipata kati ya Daraja la Kwanza na Daraja la Tatu.
Daraja
|
||||
Serikali-Kitaifa
|
Serikali-Kata
|
Binafsi-Kikristo
|
Watu- Binafsi
|
|
Daraja la I & II
|
13.8
|
1.2
|
71.9
|
2.9
|
Daraja la III
|
15.7
|
4
|
5
|
14.5
|
Daraja la IV
|
37.5
|
29.3
|
13.7
|
66.7
|
Daraja la 0
|
33.0
|
65.5
|
9.4
|
15.9
|
Sifa za waalimu kitaaluma zilipimwa katika viwango
vinne. Shule ambayo asilimia 80-100 ya waalimu wake walikuwa na shahada
ilichukuliwa kuwa na ‘sifa bora’, ilhali shule ambayo asilimia 50-79 ya waalimu
wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa nzuri’. Shule ambayo
asilimia 40-49 ya waalimu wake walikuwa na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa
ya wastani’. Nayo shule ambayo pungufu ya asilimia 40 ya waalimu wake walikuwa
na shahada ilichukuliwa kuwa na ‘sifa duni’.
Kama Kielelezo 7 kinavyoonyesha,
shule za kitaifa za serikali zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya waalimu wenye
sifa nzuri kitaaluma, zikifuatiwa na shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za
Kikristo. Shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu na watu binafsi
zilikuwa na idadi ndogo zaidi za waalimu wenye sifa nzuri kitaaluma. Mathalani,
wakati asilimia 85.7 ya waalimu katika shule za kitaifa za serikali
zilizotafitiwa na asilimia 40 ya waalimu katika shule binafsi zilizotafitiwa
zinazomilikiwa na asasi za Kikristo walikuwa na shahada, hakukuwa na mwalimu
hata mmoja aliyekuwa na shahada katika shule binafsi zilizotafitiwa
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, kati ya waalimu 303
waliotafitiwa, waalimu 11 (3.6%) tu ndio waliotoka katika shule zinazomilikiwa
na asasi za Kiislamu, waalimu 21 (6.9%) tu ndio waliotoka katika shule
zinazomilikiwa na asasi za Kikristo, na waalimu 39 (12.9%) tu ndio waliotoka
katika shule zinazomilikiwa na asasi za watu binafsi. Waalimu walio wengi
walitoka katika shule za kitaifa za serikali (116) na shule za kata za serikali
(116).
Katika kipengele hiki, zana kuu mbili za kufundishia
na kujifunzia ziliangaliwa, nazo ni maabara na maktaba. Kwa mujibu wa sera ya
taifa, kila shule ya sekondari inapaswa kuwa na maabara tatu – moja kwa
somo la fizikia, moja kwa kemia, na moja kwa biolojia. Hata hivyo, shule chache
tu ndizo zilizokuwa na maabara zote tatu. Kwa sababu hiyo, kigezo kikuu cha
uchambuzi na ulinganishi kilikuwa ni kuwepo kwa maabara walau moja na maktaba.
Kama Kielelezo 6 kinavyoonyesha, shule za kitaifa za serikali na shule binafsi
zinazomilikiwa na asasi za Kikristo pekee ndizo zilizokuwa na maabara walau
moja na maktaba.
Kulikuwa na tofauti kubwa kitakwimu katika ufaulu wa
wanafunzi kitaaluma kati ya shule zilizokuwa na maabara (X2= [N=24,
4] =18.80, p=.001, Phi=.89) na maktaba (X2= [N=24, 8]
=21.38, p=.006, Phi=.94) na zile ambazo hazikuwa nazo, hali
iliyoashiria kuwa vigezo hivi viwili vilikuwa muhimu kwa ufaulu wa wanafunzi
kitaaluma.
Jumla ya waalimu 303 walijaza hojaji. Kati yao,
asilimia 70.5 walikuwa wanaume na asilimia 29.5 walikuwa wanawake. Umri wao wa
wastani ulikuwa miaka 33.0 (Achano Kuu (SD)=9.2), nao ulianzia miaka 19 hadi
67.
Kulikuwa na mgawanyo sawa wa washiriki katika mikoa
yote iliyoshiriki, ingawa kulikuwa na idadi ya juu kidogo ya washiriki kutoka
mkoa wa Pwani (tazama Kielelezo 8). Idadi kubwa (40%) ya waalimu waliojaza hojaji
walikuwa waalimu wa masomo ya Sanaa na Sayansi za Jamii, kulinganisha na
waalimu wa Sayansi na Hisabati (37%) na waalimu wa Lugha (23%) (tazama
Kielelezo 9).
Waalimu walio wengi ama walikuwa na stashahada (38%)
au shahada (42%) ya elimu (Kielelezo 10). Zaidi ya hayo, kama Kielelezo 10
kinavyoonyesha, waalimu wengi waliojaza hojaji walikuwa na uzoefu wa kufundisha
usiozidi miaka mitano.
Ili kuchunguza ushiriki wao katika programu za
kuendeleza waalimu, waalimu waliombwa kuonyesha iwapo walipata kuhudhuria
mafunzo yoyote ya ualimu/programu zozote za kujiendeleza wakiwa kazini katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Matokeo yanaonesha kuwa asilimia 15.3 tu ya waalimu
ndio walioonyesha kuwa walipata kushiriki katika programu fulani ya
kujiendeleza kitaaluma katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Majibu
yaliyotolewa na waalimu wote, pasipo kuzingatia umiliki wa shule zao,
yalielekea kufanana kwa kiasi fulani, ingawa idadi kubwa kidogo ya waalimu wa
shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo walionesha kuwa walipata
kuhudhuria programu za kujiendeleza kitaaluma kuliko waalimu wa shule nyingine
(Kielelezo 12).
Kielelezo 12: Idadi ya waalimu walioonyesha
kuhudhuria programu za mafunzo kazini katika miaka miwili iliyopita[3]
Katika kuchunguza hamasa na mitazamo waliyo nayo
kuhusu ualimu, waalimu walipewa vifungu 19 vya maelezo na kuombwa kutoa maoni
yao kwa kuchagua jibu mojawapo kati ya majibu ya aina tano yaliyoanzia na
‘ninakubaliana sana’ hadi ‘sikubaliani kabisa’. Jedwali 3 linaeleza kwa
muhtasari matokeo hayo. Uchunguzi wa makini wa matokeo hayo ulionyesha kuwepo
sababu kuu nne kwa nini walimu wanaweza kuchagua kazi ya ualimu na kuendelea
nayo. Sababu hizo ni kama vile ‘ni rahisi kupata ajira’, ‘kwa sababu ualimu
hutoa fursa zaidi za kujiendeleza kielimu’, ‘shauku ya kusaidia wengine’ na
‘shauku ya kufundisha somo/masomo niyapendayo’. Zaidi ya asilimia 60 ya waalimu
ama ‘walikubaliana sana’ au ‘walikubaliana’ na maelezo haya.
Uchambuzi wa vigezo ulifanywa kwa kuchunguza muundo wa
ndani wa vifungu hivi 19 vya maelezo kwa lengo la kubainisha vigezo vikuu
vinavyowahamasisha waalimu kuchagua kazi ya ualimu. Vigezo vikuu vitatu
vilijitokeza, navyo ni shauku na moyo wa kupenda kusaidia wengine, kuvutiwa na
watu wengine mashuhuri, na mazingira mazuri ya kazi. Matokeo yanaonesha kuwa
‘shauku na moyo wa kupenda kusaidia wengine’ ndicho kigezo kikuu kinachoweza
kuwahamasisha walimu kuchagua kazi ya ualimu, ambapo asilimia 45 ya washiriki
walichagua kipengele hiki kuwa ndiyo sababu kuu iliyowafanya kuchagua na
kuendelea kufanya kazi ya ualimu. Kulikuwa na vifungu vikuu vinne vya maelezo
katika kipengele hiki. Vifungu hivyo ni ‘shauku ya kusaidia watu wengine’,
‘moyo wa kupenda kufanya kazi na watoto’, ‘shauku ya kufundisha somo/masomo niyapendayo’
na ‘inaendana na haiba yangu’.
Kuvutiwa na watu wengine mashuhuri ni kigezo
kilichoonesha kuwa huwahamasisha waalimu wachache zaidi kuchagua kazi ya
ualimu, ambapo asilimia 11.4 tu ya washiriki ndio walioonesha kuwa hii ndiyo
sababu iliyowafanya kuchagua kazi hii. Asilimia 16 tu ya waalimu walioshiriki
walichagua kazi ya ualimu kwa sababu kuna ‘mazingira mazuri ya kazi’ (tazama
Kielelezo 13).
% (N=)
|
||||||||||||||
Maelezo
|
Ninakubaliana Sana
|
Ninakubaliana
|
Sikubali Wala Sikatai
|
Sikubaliani
|
Sikubaliani Kabisa
|
SA+A
|
SD+D
|
|||||||
1. Ni rahisi kupata ajira
|
28.7
|
31.4
|
19.8
|
10.2
|
7.6
|
60.1
|
17.8
|
|||||||
2. Ndiyo kazi pekee niwezayo kuipata kwa sifa nilizo nazo kitaaluma
|
8.6
|
20.8
|
12.2
|
34.3
|
21.1
|
29.4
|
55.4
|
|||||||
3. Kazi ya ualimu inanipa uhakika wa ajira
|
14.9
|
25.7
|
21.5
|
20.1
|
14.2
|
40.6
|
34.3
|
|||||||
4. Kuna mshahara mkubwa
|
1.7
|
3.3
|
11.9
|
26.1
|
53.5
|
5
|
79.6
|
|||||||
5. Kuna mazingira mazuri ya kazi
|
5.0
|
16.8
|
21.8
|
26.1
|
27.1
|
21.8
|
53.2
|
|||||||
6. Inakupa hadhi kubwa katika jamii
|
4
|
17.5
|
20.8
|
28.4
|
24.1
|
21.5
|
52.5
|
|||||||
7. Ualimu unanipa matazamio mazuri ya kupata kazi
|
8.6
|
29.7
|
21.1
|
18.8
|
16.5
|
38.3
|
35.3
|
|||||||
8. Kwa kuwa ualimu hunipa fursa zaidi za kujiendeleza kielimu
|
23.8
|
37
|
14.9
|
9.6
|
10.9
|
60.8
|
20.5
|
|||||||
9. Kwa kuwa serikali inajali elimu
|
9.6
|
19.8
|
26.1
|
24.1
|
15.8
|
29.4
|
39.9
|
|||||||
10. Moyo wa kupenda kufanya kazi na watoto/vijana wadogo
|
11.6
|
29.4
|
16.8
|
20.1
|
17.5
|
41
|
37.6
|
|||||||
11. Inaendana na haiba yangu
|
13.2
|
27.7
|
25.7
|
15.5
|
13.2
|
40.9
|
28.7
|
|||||||
12. Shauku ya kusaidia watu wengine
|
30.7
|
37.3
|
13.5
|
7.9
|
7.6
|
68
|
15.5
|
|||||||
13. Shauku ya kufundisha masomo niyapendayo
|
27.1
|
37
|
13.5
|
9.9
|
9.6
|
64.1
|
19.5
|
|||||||
14. Kuvutiwa na waalimu mashuhuri
|
6.6
|
19.1
|
21.5
|
29.7
|
18.8
|
25.7
|
48.5
|
|||||||
15. Kuvutiwa na wanafamilia
|
5.9
|
16.8
|
22.1
|
29.7
|
21.5
|
22.7
|
51.2
|
|||||||
16. Kuvutiwa na wanarika wenzangu
|
3.3
|
12.5
|
19.5
|
33.7
|
27.1
|
15.8
|
60.8
|
|||||||
17. Kuvutiwa na vyombo vya habari
|
4.3
|
9.6
|
16.8
|
35
|
30.4
|
13.9
|
65.4
|
|||||||
18. Kuakisi imani yangu ya kidini
|
7.6
|
15.2
|
16.8
|
28.4
|
27.4
|
22.8
|
55.8
|
|||||||
19. Ugumu wa kupata ajira
|
10.9
|
22.8
|
24.4
|
18.2
|
20.1
|
33.7
|
38.3
|
|||||||
Pindi matokeo yalipochambuliwa kwa kuzingatia kigezo
cha umiliki wa shule, ilibainika kuwa ‘mazingiria mazuri ya kazi’ kilikuwa
ndicho kigezo muhimu zaidi kilichowavutia walimu wa shule binafsi
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu, ilhali waalimu wa shule za kitaifa za
serikali, shule za kata za serikali na shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za
Kikristo kwa kiasi kikubwa walivutiwa na vigezo vinavyohusiana na ‘shauku na
moyo wa kupenda kuwasaidia wengine’ (tazama Kielelezo 14).
Vipengele kumi na saba vilijumuishwa katika hojaji
kuchunguza moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu. Matokeo yake
yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 4 na Jedwali 5. Kwa jumla, kiwango cha
moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu kilikuwa cha chini.
Mathalani, asilimia 40.6 tu ya waalimu ndiyo ‘waliokubaliana sana’ na
‘kukubaliana’ na kauli kwamba ‘Matamanio yangu ni kuendelea kuwa mwalimu’, huku
asilimia 45.2 tu ya walimu ndio ‘wakikubaliana sana’ na ‘kukubaliana’ na kauli
kwamba ‘Ninaiona kazi ya ualimu kuwa ya kuvutia sana na yenye kuridhisha mno’.
Zaidi ya hayo, asilimia 33.7 tu ndio walioarifu kuwa
‘Ninapenda maisha ya shuleni na niko radhi kufundisha kwa maisha yangu yote’,
ilhali asilimia 35.3 tu ya waalimu ndio ‘waliokubaliana’ na kauli kuwa ‘Ikiwa
nitapewa kuchagua kazi moja tu miongoni mwa nyinginezo, bado nitachagua kuwa
mwalimu’. Kadhalika, asilimia 42.5 tu ndio ‘waliokubaliana sana’ na
‘kukubaliana’ na kauli kwamba ‘Ninaridhishwa sana na shule ninayofundisha’.
Maelezo
|
%
|
||||||
SA
|
A
|
N
|
D
|
SD
|
SA+A
|
SD+D
|
|
1. Matamanio yangu ni kuendelea kuwa mwalimu
|
12.9
|
27.7
|
22.8
|
17.5
|
17.2
|
40.6
|
34.7
|
2. Ninapenda kufundisha kuliko ilivyokuwa siku za nyuma
|
12.5
|
30.7
|
21.5
|
17.5
|
14.9
|
43.2
|
32.4
|
3. Ninapenda kufundisha somo nilipendalo kwa wanafunzi wangu
|
30.0
|
47.2
|
13.2
|
3.3
|
3.3
|
77.2
|
6.6
|
4. Niko radhi kusaidia kuendeleza shule yangu kadri niwezavyo
|
38.6
|
46.5
|
5.9
|
3.0
|
2.6
|
85.1
|
5.6
|
5. Hata wanafunzi wawe na tabia mbaya kiasi gani, bado nitajaribu kadri
niwezavyo kuwafundisha
|
38.6
|
37.0
|
8.9
|
6.6
|
5.0
|
75.6
|
11.6
|
6. Ninaiona kazi ya ualimu kuwa ya kuvutia sana na yenye kuridhisha mno
|
16.5
|
29.7
|
18.5
|
17.2
|
14.2
|
46.2
|
31.4
|
7. Kazi ya ualimu ilikuwa/ni mojawapo ya machaguo yangu matatu ya kwanza
ya kazi
|
22.1
|
36.3
|
15.5
|
11.9
|
10.6
|
58.4
|
22.5
|
8. Ualimu ni mgumu mno na hakuna faida ya maana unayoipata
|
23.8
|
24.8
|
17.5
|
18.8
|
12.2
|
48.6
|
31.0
|
9. Mitazamo na tabia za wanafunzi zimefifisha shauku yangu ya kufundisha
|
11.6
|
22.1
|
17.5
|
31.7
|
13.2
|
33.7
|
44.9
|
10. Kazi ya kufundisha ni ngumu mno kwangu na ninataka kuachana nayo
|
7.9
|
12.2
|
20.8
|
35.6
|
20.1
|
20.1
|
55.7
|
11. Ninapenda maisha ya shuleni na niko radhi kufundisha kwa maisha yangu
yote
|
10.9
|
22.8
|
23.1
|
24.8
|
15.2
|
33.7
|
40.0
|
12. Sijakata tamaa; ninayo malengo ninayotaka kuyatimiza katika ualimu
|
14.9
|
17.8
|
18.8
|
27.7
|
17.5
|
32.7
|
45.2
|
13. Hata kukiwa na kazi nzuri zaidi, nitaendelea kufundisha
|
29.0
|
19.5
|
18.5
|
17.5
|
12.5
|
48.5
|
30.0
|
14. Kuthaminiwa kwangu na shule/mkuu wa shule kulinichochea kufanya kazi
|
10.9
|
30.0
|
23.8
|
16.8
|
13.9
|
40.9
|
30.7
|
15. Ikiwa nitapewa kuchagua kazi moja tu miongoni mwa nyinginezo, bado
nitachagua kuwa mwalimu
|
10.2
|
25.1
|
24.4
|
18.2
|
18.2
|
35.3
|
36.4
|
16. Ninaridhishwa sana na shule ninayofundisha
|
15.5
|
37.0
|
21.8
|
12.5
|
10.2
|
52.5
|
22.7
|
17. Kwa jumla, ninapenda kuwafundisha wanafunzi wangu
|
32.0
|
46.5
|
11.2
|
4.0
|
3.6
|
78.5
|
7.6
|
Alama za wastani
|
19.9
|
30.2
|
17.9
|
16.7
|
12.0
|
50.0
|
28.8
|
Uchambuzi wa vigezo ulifanywa kuchunguza miundo ya
ndani ya viwango vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu ambapo vipengele hivi
17 vilifanyiwa uchambuzi wa sehemu kuu. Sehemu kuu tatu zilijitokeza zikiakisi
hali tatu za viwango vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu. Hali hizo tatu ni
‘moyo wa kujitolea walio nao waalimu na kuridhika kwao na kazi ya ualimu’,
‘moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kuwasaidia wanafunzi’ na ‘moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa shule na kuridhika kwao na shule’. Matokeo yake
yameelezwa kwa muhtasari katika Kielelezo 15 na Kielelezo 16. Kielelezo 15
kinaonesha kiwango cha jumla cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika
hali zote tatu na Kielelezo 16 kinaonyesha kiwango cha moyo wa kujitolea walio
nao waalimu kwa kuzingatia kigezo cha umiliki wa shule.
Kama Kielelezo 15 kinavyoonyesha, waalimu waliarifu
kuwa na moyo wa kujitolea wa hali ya juu katika kuwasaidia wanafunzi, ambapo
asilimia 80.1 ya waalimu waliarifu kuwa na moyo wa kuwasaidia wanafunzi.
Kiwango cha moyo wa kujitolea kwa kazi ya ualimu kilikuwa cha chini sana ambapo
asilimia 36.6 tu ya waalimu ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea na
walioridhika na kazi ya ualimu. Hali kadhalika, kiwango cha moyo wa kujitolea
kwa ajili ya shule kilikuwa cha chini, ambapo asilimia 42.4 tu ya waalimu ndio
walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili ya shule walizokuwa
wakifundisha.
Kielelezo 15: Idadi ya waalimu walioarifu
kuwa na moyo wa kujitolea katika vipengele mbalimbali vya kazi ya ualimu
Uchambuzi ulifanywa kuchunguza kiwango cha moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia kigezo cha umiliki wa shule. Hii
ilifanywa kwa kulinganisha kiwango cha moyo wa kujitolea na kuridhishwa na kazi
ya ualimu miongoni mwa waalimu wa shule za serikali na za binafsi. Matokeo yake
yameelezwa kwa muhtasari katika Kielelezo 16. Kwa jumla, waalimu wa shule
binafsi za Kikristo walionyesha kuwa na moyo wa kujitolea wa hali ya juu na
walioridhishwa na kazi ya ualimu kuliko waalimu wa shule nyinginezo. Mathalani,
wakati asilimia 73 ya waalimu katika shule binafsi za Kikristo waliarifu kuwa
na moyo wa kujitolea na kuridhishwa na kazi ya ualimu, pungufu ya asilimia 55
ya waalimu wa shule nyinginezo ndio walioarifu kuwa na moyo wa kujitolea na
kuridhishwa na kazi ya ualimu.
Kiwango cha moyo wa kujitolea wa waalimu kwa shule
walizofanyia kazi kilikuwa cha chini zaidi miongoni mwa waalimu wa shule
binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi na wale wa shule za kata za serikali,
lakini kilikuwa cha juu kwelikweli miongoni mwa waalimu wa shule binafsi za
Kikristo. Mathalani, wakati asilimia 71 ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo
waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizofundisha,
asilimia 32 tu ya waalimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi ndio
walioarifu hivyo. Asilimia 36 tu ya waalimu wa shule za kata za serikali na
asilimia 46 tu ya waalimu wa shule za kitaifa za serikali ndio walioarifu kuwa
na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa wakifundisha. Kwa
kiasi fulani kulikuwepo pia na moyo wa kujitolea wa hali ya juu kwa shule
miongoni mwa waalimu wa shule binafsi za Kiislamu, ambapo asilimia 56 ya
waalimu wa shule hizi waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na
shule walizofundisha.
Kwa jumla, na kwa wastani, asilimia 58.6 tu ya walimu
walioshiriki katika utafiti ndio walioarifu kuwa walikuwa wameridhika na
mazingira ya kazi katika shule walizokuwa wakifundisha. Pindi uchambuzi
ulipofanywa kwa kuzingatia kigezo cha shule, kama Kielelezo 17 kinavyoonyesha,
matokeo yalionyesha kuwa idadi kubwa zaidi kitakwimu (X2=[N=297,
12]=49.9, p<.0005) ya walimu wa shule binafsi zinazomilikiwa na
asasi za Kikristo (95%) na wale wa shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za
Kiislamu (82%) waliarifu kuridhishwa na mazingira ya kazi ya shule zao
kulinganisha na waalimu wa shule za kitaifa za serikali (59%), shule za kata za
serikali (51%) na shule binafsi zinazomilikiwa na watu binafsi (51%).
Uchambuzi ulifanywa pia kuchunguza kiwango cha moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia jinsia yao. Cha kushangaza, ingawa
tofauti haikuwa kubwa kitakwimu, idadi kubwa ya waalimu wa kiume waliarifu kuwa
walikuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na masuala mbalimbali kuliko
waalimu wenzao wa kike. Mathalani, kwa jumla, asilimia 55.4 ya waalimu wa kiume
waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na kuridhika na kazi ya ualimu kulinganisha
na asilimia 46 ya waalimu wa kike.
Pindi uchambuzi ulipofanywa kwa kuzingatia vipengele
vitatu vya moyo wa kujitolea walio nao waalimu, matokeo yalionyesha mwelekeo
unaofanana huku idadi kubwa ya waalimu wa kiume wakiarifu kuwa na moyo wa
kujitolea kwa masuala mbalimbali katika kazi ya ualimu kuliko waalimu wa kike.
Mathalani, asilimia 38.5 ya waalimu wa kiume waliarifu
kuwa na moyo wa kujitolea na wenye kuridhika na kazi ya ualimu, kulinganisha na
asilimia 27 ya waalimu wa kike. Zaidi ya hayo, wakati asilimia 82 ya waalimu wa
kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea kuwasaidia wanafunzi, asilimia 76.5
ya waalimu wa kike ndio walioarifu hivyo. Kadhalika, asilimia 45.8 ya waalimu
wa kiume waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule walizokuwa
wakifundisha kulinganisha na asilimia 34.9 ya waalimu wa kike (tazama Kielelezo
18).
Uchambuzi ulifanywa kuchunguza kiwango cha moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa kuzingatia uzoefu wa kufundisha na masomo ya
kufundisha. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 5.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa, kwa wastani, waalimu wa
masomo ya lugha walikuwa na moyo wa kujitolea zaidi na walioridhika zaidi na
kazi ya ualimu kuliko walimu wa masomo ya sanaa na ya sayansi. Mathalani,
asilimia 85.4 ya waalimu wa masomo ya lugha waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea
katika kuwasaidia wanafunzi, kulinganisha na asilimia 78.1 ya waalimu wa masomo
ya sanaa na asilimia 79.6 ya walimu wa sayansi. Kadhalika, asilimia 45.1 ya
waalimu wa masomo ya lugha waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika
na shule walizokuwa wakifundisha, kulinganisha na asilimia 37.3 ya waalimu wa
sayansi na asilimia 44.8 ya waalimu wa masomo ya sanaa. Lakini, idadi kubwa
(39.9%) ya waalimu wa sayansi waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na
walioridhika na kazi ya ualimu kuliko waalimu wa lugha (35.4%) na waalimu wa
masomo ya sanaa (34.9%). Hata hivyo, uchambuzi uliofanywa kwa njia ya chi-squareulionyesha
kutokuwepo kwa tofauti kubwa kitakwimu miongoni mwa makundi haya matatu ya
waalimu.
Walimu kuwa na sifa nzuri kitaaluma hakukuashiria kwa
namna mbalimbali kuwa na sifa ya moyo wa kujitolea katika kufundisha, kwani
waalimu wenye sifa za kiwango cha chini waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea wa
hali ya juu katika kufundisha kuliko waalimu wenye sifa za kiwango cha juu.
Mathalani, idadi kubwa kitakwimu (64.3%) ya waalimu wa ngazi ya cheti waliarifu
kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na kazi ya ualimu kuliko wale wa
ngazi ya stashahada (40.1%) na shahada (28.4%). Kadhalika, asilimia 93.3 ya
waalimu wenye cheti cha ualimu waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea kuwasaidia
wanafunzi, kulinganisha na asilimia 75.5 ya waalimu wenye stashahada na
asilimia 79.6 ya waalimu wenye shahada. Hata hivyo, idadi kubwa ya waalimu wa
ngazi ya shahada waliarifu kuwa na moyo wa kujitolea na walioridhika na shule
walizokuwa wakifundisha kuliko waalimu wa ngazi ya stashahada (38.3%) na wa
ngazi ya cheti (35.7%).
Masomo ya kufundisha
|
Uzoefu wa kufundisha
|
|||||||
Sanaa
|
Lugha
|
Sayansi
|
p
|
Stashahada
|
Shahada
|
Cheti
|
p
|
|
1. Moyo wa kujitolea na kuridhika na kazi ya ualimu
|
34.9
|
35.4
|
39.9
|
0.70
|
40.1
|
28.4
|
64.3
|
0.03
|
2. Moyo wa kujitolea kusaidia wanafunzi
|
78.1
|
85.4
|
79.6
|
0.90
|
75.5
|
79.6
|
93.3
|
0.68
|
3. Moyo wa kujitolea kwa shule na kuridhika na shule
|
44.8
|
45.1
|
37.3
|
0.45
|
38.3
|
44.5
|
35.7
|
0.28
|
Uongozi wa shule ni kigezo muhimu kinachoukilia
kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kufundisha. Katika
utafiti huu, tuliwaomba waalimu kutathmini uongozi wa shule zao katika
vipengele mbalimbali. Walipewa vifungu 12 vya maelezo na kuombwa kutathmini ni
kwa kiasi gani walikubaliana na maelezo hayo kwa kuchagua jibu mojawapo kati ya
majibu ya aina tano yaliyoanzia na ‘ninakubaliana sana’ hadi ‘sikubaliani
kabisa’. Matokeo yake yameelezwa kwa muhtasari katika Jedwali 6 na Kielelezo
19.
Kama Kielelezo 19 kinavyoonyesha, ukiacha waalimu wa
shule binafsi za Kikristo, maoni ya waalimu kuhusu kiwango cha ubora wa uongozi
wa shule zao yalionyesha kuwa kilikuwa cha chini kabisa. Mathalani, kwa
wastani, wakati asilimia 79.8 ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo waliarifu
kuwa uongozi wa shule zao ulikuwa ni wenye ufanisi katika masuala mbalimbali,
asilimia 48 tu ya waalimu wa shule za kata za serikali, asilimia 37.9 tu ya
waalimu wa shule binafsi za Kiislamu na asilimia 47 tu ya waalimu wa shule
zinazomilikiwa na watu binafsi ndio waliokuwa na maoni sawa na hayo. Hivyo,
ingawa tofauti haikuwa kubwa kitakwimu (X2= [N=266, 16]=16.82, p=.40),
kulikuwa na tofauti za wazi kabisa katika maoni kuhusu ufanisi wa uongozi wa
shule miongoni mwa waalimu wa shule za makundi hayo matano, ambapo idadi kubwa
ya waalimu wa shule binafsi za Kikristo walikuwa na maoni yaliyounga mkono
uongozi wa shule zao kuliko waalimu wa shule nyingine.
Kadhalika, pindi uchambuzi ulipofanywa kwa kuzingatia
vipengele kadhaa, waalimu wa shule binafsi za Kikristo walipata alama za juu
mno kuliko waalimu wa shule nyingine. Mathalani, wakati asilimia 76.2 ya
waalimu wa shule binafsi za Kikristo ‘walikubaliana sana’ na pia
‘walikubaliana’ na mtazamo kwamba uongozi wa shule zao ‘hutengeneza mazingira
mazuri ya kazi’, asilimia 49.1 tu ya waalimu wa shule za kitaifa za serikali,
asilimia 37 tu wa shule za kata za serikali, asilimia 45.5 tu ya waalimu wa
shule binafsi za Kiislamu na asilimia 35.9 tu ya waalimu wa shule za watu
binafsi ndio waliokuwa na maoni sawa na hayo. Jambo la kuvutia, hata hivyo, ni
kwamba idadi kubwa ya waalimu wa shule binafsi za Kiislamu walikuwa na maoni
chanya kuhusu vipengele viwili vya kupima ufanisi wa uongozi wa shule, navyo ni
‘(uongozi wa shule) husisitiza nidhamu ya kiwango cha juu’ na ‘(uongozi wa
shule) ni mfano wa kuigwa’. Mathalani, asilimia 72.7 ya waalimu wa shule hizi
‘walikubaliana sana’ au ‘walikubaliana’ na kauli kwamba uongozi wa shule zao
‘ni mfano wa kuigwa’.
% ‘Ninakubaliana Sana’ na ‘Ninakubaliana’
|
|||||
Maelezo
|
Serikali-Kitaifa
|
Serikali-Kata
|
Binafsi-Kikristo
|
Binafsi-Kiislamu
|
Binafsi-Watu
|
1. Hutengeneza mazingira mazuri ya kazi
|
49.1
|
37.0
|
76.2
|
45.5
|
35.9
|
2. Huhakikisha kuna umoja/ushirikiano baina ya uongozi/ waalimu/
watumishi/ jamii
|
57.7
|
54.3
|
81.0
|
18.2
|
48.7
|
3. Una mipango kabambe, utaratibu mzuri
|
55.2
|
49.1
|
85.7
|
0
|
46.2
|
4. Huhamasisha kushiriki katika kuendesha masuala ya shule
|
52.7
|
53.4
|
81.0
|
27.3
|
48.8
|
5. Huchochea ushirikiano
|
60.3
|
48.3
|
85.7
|
45.5
|
59.0
|
6. Huruhusu kupata taarifa kirahisi
|
55.2
|
49.1
|
76.2
|
27.3
|
50.0
|
7. Huonyesha kuwa na sifa za juu za uongozi
|
50.9
|
44.8
|
66.6
|
27.3
|
51.3
|
8. Hufanya tathmini ya mara kwa mara na ya haki kwa watumishi
|
54.3
|
45.7
|
76.2
|
36.4
|
38.5
|
9. Huhakikisha kuna vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia
|
55.2
|
48.3
|
76.2
|
45.5
|
41.0
|
10. Husisitiza nidhamu ya kiwango cha juu
|
62.1
|
56.9
|
90.5
|
72.7
|
56.4
|
11. Ni mfano wa kuigwa
|
51.8
|
43.1
|
80.9
|
72.8
|
43.6
|
12. Huonyesha sifa za kuigwa za mwalimu mzuri
|
60.4
|
46.5
|
81.0
|
36.4
|
53.8
|
Wastani
|
55.4
|
48.0
|
79.8
|
37.9
|
47.8
|
Kielelezo 19: Idadi ya waalimu ‘waliokubaliana
sana’ na ‘waliokubaliana’ na kauli kuwa uongozi wa shule yao una ufanisi
3.4 Muhtasari: Uhusiano uliopo baina ya ufaulu wa shule kitaaluma na sifa za
walimu kitaaluma, moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu na maoni yao kuhusu
ufanisi wa uongozi wa shule
Kwa matokeo ya hapo juu, ni dhahiri kuwa vipengele
vitatu vinaonyesha kuwa ni muhimu zaidi katika kuukilia ufaulu wa shule
kitaaluma. Vipengele hivyo ni sifa za waalimu kitaaluma, moyo wa kujitolea
walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu na mtazamo wao chanya kuhusu ufanisi wa
uongozi wa shule. Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha dhahiri kuwa waalimu wenye
sifa nzuri kitaaluma wanao uwezo wa kuwafanya wanafunzi kufaulu vizuri, lakini
hii inawezekana ikiwa tu vigezo vingine vitatiliwa maanani, navyo ni moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa kazi yao na vilevile kuridhishwa kwao na uongozi
wa shule. Hii ina maana kuwa kuboresha sifa za waalimu kitaaluma hakuna budi
kwenda bega kwa bega na kuboresha mazingira ya kazi ya waalimu na ufanisi wa
uongozi wa shule ili waalimu waweze kuifurahia kazi yao na hivyo kuboresha moyo
wao wa kujitolea kazini.
Hata hivyo, pindi uchambuzi ulipofanywa kwa njia
ya chi-square, moyo wa kujitolea walio nao waalimu na maoni yao
kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule ndivyo vigezo pekee vilivyoonyesha kuleta
matokeo muhimu kitakwimu.
Ili kutimiliza utafiti uliofanywa kwa njia ya hojaji,
waalimu walipewa fursa ya kubadilishana uzoefu wao kuhusu kazi ya ualimu na
mazingira yao ya kazi kwa jumla kupitia majadiliano ya vikundi lengwa.
Majadiliano yalifanywa kwa kikundi walau kimoja katika kila shule iliyoshiriki,
na kila kikundi kilikuwa na washiriki kuanzia watano (5) hadi tisa (9).
Majadiliano haya ya vikundi lengwa yalirekodiwa kwenye vinasa sauti na
kunakiliwa neno kwa neno katika maandishi. Kisha majadiliano yaliyonakiliwa
yalifanyiwa uchambuzi wa kimaudhui, ambapo maudhui makuu yalibainishwa na
kufafanuliwa kwa kutumia nukuu za washiriki.
Maudhui makuu manne yalibainishwa, nayo ni: (i) kwa
nini waalimu walichagua kazi ya ualimu; (ii) mitazamo ya waalimu kuhusu kazi ya
ualimu; na (iii) maoni ya waalimu kuhusu sababu za wanafunzi kufanya vibaya
kitaaluma na nini kifanyike kuboresha kiwango cha elimu na kiwango cha
ufundishaji.
Uchambuzi wa majadiliano ya vikundi lengwa ulibainisha
sababu kuu tano zilizowavutia waalimu kuchagua kazi ya ualimu. Sababu ya kwanza
na iliyo muhimu zaidi ni urahisi wa kupata ajira waliouona waalimu baada ya
kuhitimu mafunzo. Waalimu wengi walieleza kwamba walichagua kazi ya ualimu kwa
sababu waliamini kuwa ingekuwa rahisi kwao kupata ajira baada ya kumaliza
masomo yao kulinganisha na kazi nyingine. Walimu walieleza pia kwamba kazi ya
ualimu iliwapa uhakika mkubwa zaidi wa kusaidia familia zao kwani kuna uhakika
wa kupata ajira mara tu mtu anapohitimu mafunzo yake. Nukuu za maoni ya baadhi
ya washiriki zilizopo hapa chini zinathibitisha hili:
Nadhani sababu kubwa iliyonifanya kuchagua kazi hii
(ualimu) ilikuwa ni ukweli kwamba nilifikiri itakuwa rahisi kupata ajira baada
ya masomo yangu. Lakini kama ingewezekana kupata ajira katika fani nyingine,
kamwe nisingeweza kuchagua kazi ya ualimu (Mwalimu, Shule A1, Mkoa wa Pwani).
Nilichagua kuwa mwalimu kwa sababu nilijua ilikuwa
rahisi kupata kazi katika sekta ya elimu. Nina ndugu wengi ambao walisomea kozi
nyingine na niliwaona walivyohangaika kupata ajira; sikutaka kuhangaika kama
wao, kwa hiyo nikaamua kuwa mwalimu. Lakini ualimu siyo kazi ninayopanga
kuifanya kwa muda mrefu; mwishowe nitaachana na kazi hii (Mwalimu, Shule Z,
Mkoa wa Pwani).
Kwa kweli, nilikuwa mwalimu kwa bahati mbaya tu! Ni
kwa sababu ilikuwa rahisi zaidi kwangu kupata kazi. Lakini, kwa kweli, baada ya
kujiunga na kazi hii, hakuna kitu ambacho kweli kinanihamasisha kuendelea kuwa
mwalimu. Ni suala la wakati tu; bila shaka nitaachana na kazi hii (Mwalimu, Shule
H, Mkoa wa Dodoma).
Mtu asikudanganye. Tupo hapa kwa sababu tulitaka ajira
na ualimu ndiyo njia rahisi zaidi ya kupata kazi (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa
Singida).
Sababu ya pili iliyotajwa mara kwa mara kama kigezo
kilichowafanya waalimu kuchagua kazi hii ilikuwa ni kutokuwa na sifa za
kujiunga na kazi nyingine. Waalimu walieleza kuwa baadhi yao walichagua kazi ya
ualimu baada ya kushindwa kupata sifa zinazohitajika kujiunga na kazi nyingine,
kama vile katika sekta ya fedha, uchumi, tiba, uhandisi, na kadhalika. Hivyo,
waliona kuwa kazi ya ualimu ingekuwa njia ya kupatia kazi nyingine wazipendazo.
Kwa sababu hiyo, ualimu ulichukuliwa zaidi kuwa ni kazi ‘ya mpito tu’ wakati
mtu akisubiria kazi nyingine nzuri ijitokeze. Ni dhahiri kuwa hali hii
huwafanya waalimu kutojihusisha sana na kazi ya ualimu na kutokuwa na moyo wa
kujitolea kwa kazi hii. Nukuu chache za maoni zilizopo hapa chini
zinathibitisha hili:
Watu huchagua kazi hii (ualimu) kama chaguo la mwisho
– wameshindwa kupata kitu kingine chochote cha maana maishani mwao na, kwa
hiyo, kazi ya ualimu ndilo chaguo pekee lililobaki. Mimi ni mfano halisi: niko
hapa kwa sababu matokeo yangu ya kidato cha sita yalikuwa ovyo. Nilitaka
kusomea Uchumi, lakini matokeo yangu hayakuniruhusu. Vinginevyo, kamwe
nisingekuwa mwalimu (Mwalimu, Shule Z1, Mkoa wa Pwani).
...Halafu, hii ndiyo kazi pekee ambayo mtu yeyote
anaweza kujiunga nayo. Ukifeli, huku ndiko unakoishia. Kwa hiyo niko hapa kwa
sababu, kwa kweli, nilishindwa kupata matokeo mazuri ya kujiunga na kazi
nyingine. Ningeenda wapi kwingine na matokeo yangu mabaya kwa kila somo
nililofanya? Kwa mfano, nilikuwa na ‘credit’ mbili tu, zote zilikuwa ‘E’;
ningeenda wapi kwingine kama siyo Diploma ya Ualimu? (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa Singida)
Ualimu haukuwa chaguo langu la kwanza. Chaguo langu la
kwanza lilikuwa utalii, na nilichagua ualimu kama chaguo la tatu.
Nililazimishwa kuwa mwalimu; walinipa chaguo la tatu. Tangu hapo nimekuwa sina
furaha (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).
Kwa upande wangu, nilijiunga na kazi ya ualimu kwa
sababu nilipata Daraja la Tatu na sikupata alama nzuri za kuniwezesha kujiunga
na kidato cha tano, kwa hiyo ilibidi niende Diploma ya Ualimu. Kwa hiyo ualimu
haukuwa chaguo langu hata kidogo, lakini mazingira yamenilazimisha kujiunga nao
kwa sababu ya matokeo yangu mabaya. Lakini kama kitu kingine kizuri
kikijitokeza, nitaachana mara moja na kazi hii bila kujiuliza maswali (Mwalimu,
Shule J, Mkoa wa Dodoma).
Ingawa waalimu wengi walioshiriki katika majadiliano
haya ya vikundi walitaja sifa duni kitaaluma na urahisi wa kupata ajira kuwa
ndizo sababu kuu zilizowavutia kuchagua kazi ya ualimu, waalimu wengine
wachache walitaja sababu nyingine kama vile ‘kupenda kwa mtu na kuvutiwa na
watu wengine mashuhuri’. Baadhi ya waalimu walieleza kwamba walichagua kazi ya
ualimu kwa sababu waliipenda kazi hii na waliamini ilikuwa ndiyo njia bora
zaidi ya kuitumikia jamii. Aidha, waliiona kazi ya ualimu kuwa ni kazi ya
uadilifu iliyohitaji watu waadilifu.
Waalimu wengine walieleza kuwa walichagua kazi ya
ualimu kwa sababu ya kuvutiwa na wazazi na/au ndugu wengine wa karibu. Walidai
kwamba walichagua kazi ya ualimu kwa sababu tu wazazi wao au watu wengine wa
karibu waliokuwa wa muhimu kwao walikuwa waalimu. Zaidi ya hayo, waalimu
wengine walisema kuwa walichagua kazi ya ualimu kwa sababu walishauriwa kufanya
hivyo na watu wengine wa muhimu kwao. Hapa chini kuna baadhi ya nukuu
zinazothibitisha maoni hayo:
Ninaipenda Historia, na niliona kwamba kuwa mwalimu wa
Historia ingekuwa ni njia bora zaidi ya kupanua maarifa yangu katika eneo hili
(Mwalimu, Shule J, Mkoa wa Dodoma).
Ninapenda tu kufundisha wengine; kwa hiyo kujiunga na
kazi ya ualimu lilikuwa ni chaguo langu kwa asilimia mia moja kwa sababu
ninapenda ualimu (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).
Kwangu mimi, ni kwa sababu nilivutiwa na mazingira
niliyokuwemo. Kijiji ninachotoka ualimu ndiyo kazi pekee ambayo watu wanaijua,
kwa hiyo kila mtu ni kama anapenda ualimu, na mimi ni zao lake (Mwalimu, Shule
M, Mkoa wa Kigoma).
‘Nilirithi’ kutoka kwa wazazi wangu. Wazazi wangu
wote, baba na mama, ni waalimu na nilikua nikiwa ninaupenda ualimu, na kwa
kweli nina furaha kuwa mwalimu (Mwalimu, Shule T, Mkoa wa Mtwara).
Siipendi kazi ya ualimu. Nilitaka kusomea utawala,
lakini wazazi wangu walinishauri kusomea elimu maalumu, nikakubali na nilikuwa
ninategemea kwamba ningefundisha watoto wenye mahitaji maalumu. Lakini nipo
hapa, nikifanya mambo ambayo kamwe sikutaka kuyafanya. Badala ya kunipeleka
kwenye shule maalumu ambako ningeweza kufundisha wanafunzi wenye ulemavu,
walinileta hapa, na kunilazimisha kufundisha somo ambalo kamwe sikulitaka
(Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).
Uchambuzi wa majadiliano ya vikundi lengwa vya waalimu
ulionyesha masuala kadhaa yanayoweza kuchukuliwa kuwa ndiyo mitazamo waliyo
nayo kuhusu kazi ya ualimu. Mitazamo hiyo inaweza kuwekwa katika makundi makuu
mawili, nayo ni mitazamo chanya na mitazamo hasi. Hapa tutaonyesha baadhi ya
mitazamo iliyo muhimu.
Mitazamo chanya (sababu zinazotia hamasa)
Mitazamo kadhaa chanya au sababu zinazotia hamasa
kuhusu kazi ya ualimu zilibainishwa katika majadiliano haya. Kwanza, waalimu
walieleza kwamba walifurahia ukweli kwamba kazi ya ualimu iliwapa fursa ya
kuendelea kujifunza. Walidai kuwa ni ualimu pekee unaomwezesha mtu kujifunza na
kuongeza upeo wa maarifa yake kila mara. Pili, waalimu walibainisha pia ukweli
kwamba ilikuwa rahisi zaidi kwa waalimu kujiendeleza zaidi kimasomo
kulinganisha na kazi nyingine. Hivyo basi, hali hii iliwapa uwezekano wa
kujiendeleza katika kazi zao na vilevile urahisi wa kubadili kazi. Tatu, waalimu
waliona kuwa walisikia faraja pindi kazi yao ilipothaminiwa, hususan na
wanafunzi waliowafundisha. Waliona kuwa wanafunzi wengi walithamini kazi yao.
Nne, uwezekano wa kukutana na watu mbalimbali na kujipatia marafiki wapya
ulichukuliwa kuwa ni jambo chanya. Hapa chini kuna baadhi ya nukuu
zinazothibitisha mitazamo hiyo:
Ualimu umekuwa mzuri kwangu kwa sababu ninapata
marafiki na kukutana na watu wapya kila siku. Vilevile unatupatia fursa ya
kujua maisha halisi ya Tanzania: nimeona jinsi nchi hii ilivyo maskini na
tajiri kupitia kwa watoto ninaowafundisha. Huu ni uzoefu mzuri kwangu mimi
(Mwalimu, Shule Z1, Mkoa wa Pwani).
Kitu kizuri kuhusu ualimu ni kwamba inabidi usome kila
siku. Aina ya watoto tunaowafundisha siku hizi ‘inatulazimisha’ kusoma. Kwa
kuwa wanajua mambo mengi, usipopiga msasa akili yako, utakuwa kichekesho
darasani. Kwa hiyo katika ualimu inabidi usome kila siku na hii ni nzuri kwangu
(Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara).
Wakati pekee ninaoufurahia katika kazi hii ni pale
ninapoona wanafunzi wangu wakifanya vizuri katika somo langu, nitaenda
kuwaambia wenzangu na pale unapoonana na mkuu wa shule na kuona anatabasamu; na
hii inanifanya nijisikie vizuri (Mwalimu, Shule H, Mkoa wa Dodoma).
Inaleta faraja; ni vizuri kujua kuwa na mimi pia
ninachangia kuboresha maisha ya mtu na kwamba mimi pia ninajenga taifa
(Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida).
Mitazamo hasi (sababu zinazovunja moyo)
Walimu walibainisha mitazamo mingi hasi katika kazi ya
ualimu, ambayo pia inaweza kuelezwa kuwa ni sababu zinazoondoa hamasa au sababu
‘zinazovunja moyo’. Mitazamo hii kwa kiasi kikubwa ilihusu maeneo makuu mawili,
nayo ni mazingira duni ya kazi na mtazamo hasi kuhusu kazi ya ualimu (walio nao
wanajamii, wanafunzi na hata serikali). Hapa chini tumeonyesha na kufafanua baadhi
ya hisia muhimu za moyoni walizo nazo waalimu kuhusu maeneo haya.
Walimu wengi walilalamika kwamba wanafunzi wao
hawawapi heshima wanayostahili walimu wao na walikuwa na mitazamo hasi sana
kuhusu kazi ya ualimu. Hii ilijitokeza zaidi katika baadhi ya shule binafsi
ambazo huchukua wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo. Kwa mujibu wa
waalimu, wanafunzi wa shule hizi waliamini kuwa waalimu wao wanafanya kazi ya
ualimu kwa sababu ni maskini. Hapa chini kuna maoni ya baadhi ya waalimu kuhusu
suala hili:
...wanafunzi wananiona kama ‘nimechemsha’, mtu ambaye
nimepotea. Wanaamini mwalimu ni mtu maskini, hana mwelekeo maishani. Kuna
wakati wanafunzi wananiuliza, “Mwalimu, una akili sana, lakini sasa kwa nini
uliamua kuwa mwalimu?” Maswali ya aina hii yanakera. Ina maana wanaamini
mwalimu ni mtu aliyefeli, asiye na akili. Ninapowaambia, “Nilipenda tu kuwa
mwalimu”, wananiambia, “Huoni kwamba ‘unachelewa katika maisha’?” Haya ndiyo
maisha tunayoishi katika shule hii (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).
Ahaa, haa! Ngoja nikuambie kitu ... kuna mwanafunzi
mmoja darasani mwangu ambaye ana akili kwelikweli. Siku moja, ehee,
nilimwambia, “Utakuwa mwalimu mzuri sana.” Kauli hiyo ilimfanya alie sana.
Nikashangaa kwa nini analia. Baadaye akaniambia kamwe hataki kuwa mwalimu, na
kwamba nilikuwa ninamtakia mabaya kumwambia atakuwa mwalimu mzuri. Nilijisikia
vibaya sana (Mwalimu, Shule Z, Mkoa wa Pwani).
Ama kuhusu mitazamo ya jamii na serikali kuhusu
waalimu, waalimu walisema:
Hii ni kazi ngumu sana. Hakuna anayejali – si jamii
ambako unafundisha, si serikali. Jamii inatuona tumepotea, hatuna la maana na
tutaishia kushindwa. Jamii inafanya maisha yetu hapa kuwa ya ovyo sana kwa
sababu hawathamini kile tunachokifanya. Halafu, mzazi wetu, serikali, ndiyo
mbaya zaidi. Wanawatupa tu mashuleni, wanaacha hivyo tu. Hakuna anayejali –
hakuna nyumba, hakuna usafiri. Unahangaika hata kupata mshahara wako; wala
sizungumzii mishahara kuwa midogo sana. Kuchagua kuwa mwalimu ni kuchagua
kuhangaika maisha yako yote (Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida).
Pengine sababu zinazovunja moyo zilizobainishwa zaidi
ni zile zilizohusiana na mazingira duni ya kazi kama yanavyodhihirishwa na
kuwepo kwa mishahara midogo na ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia.
Waalimu wengi walizungumza kwa ukali kuhusu mishahara midogo waliyolipwa, na
vilevile ukweli kwamba shule nyingi hazikuwa na zana muhimu za kufundishia.
Waalimu pia ‘walilia’ kwa ukali kuhusu ukosefu wa programu za mafunzo kazini.
Huku wakikosoa zaidi, walisema kuwa pindi fursa za aina hiyo zinapotokea, wakuu
wa shule zao ndio wanaohudhuria kwani zina marupurupu.
3.5.4 Mitazamo ya
waalimu kuhusu wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma na nini kifanyike kuboresha
kiwango cha elimu
Katika sehemu ya mwisho ya majadiliano ya vikundi
lengwa, washiriki waliombwa kubainisha mambo waliyodhani kuwa yalisababisha
wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya taifa, hususan wakitilia maanani
Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka jana. Waliombwa pia
kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kurekebisha hali hiyo na kuboresha
kiwango cha elimu nchini kwa jumla.
Mambo makuu mawili yalibainishwa kuwa ndiyo
husababisha wanafunzi kufanya vibaya. Kwanza, waalimu walio wengi walitaja
mazingira duni ya kazi kuwa ndiyo sababu kuu ya kufanya vibaya. Waalimu
walieleza bayana kwamba kwa mazingira duni ya kazi yaliyopo, waalimu hawakuwa
wakifundisha kwa uwezo wao wote na kwamba mazingira ya shule yalikuwa
yakiwavunja moyo katika kutimiza wajibu wao kwa ukamilifu na kwa
ufanisi. Masuala makuu matatu yalitajwa bayana kuwa yalisababisha kuwepo
kwa mazingira duni ya kazi. Masuala hayo ni uduni wa mishahara na marupurupu
mengine ya waalimu, ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia na uongozi na
usimamizi mbaya wa shule.
Pengine mishahara duni ndiyo sababu iliyokuwa
ikiwavunja moyo zaidi waalimu walio wengi. Walidai, kwa mfano, kuwa mwalimu
mwenye shahada alikuwa akipata mshahara ulio pungufu ya shilingi 500,000/-
anapoajiriwa kwa mara ya kwanza, nao wakajiuliza ni waajiriwa wengine wangapi
wa serikali wenye kiwango cha elimu kilicho sawa na hicho ambao humudu
kuendesha maisha yao kwa mwezi kwa kiwango hiki cha mshahara? Walisema vilevile
kwamba, licha ya mishahara midogo waliyokuwa wakiipata, kuna makato mengi
yanayozidi kupunguza kipato halisi wanachopokea.
Vilevile kulikuwa na suala la kupandishwa madaraja
kazini. Waalimu wengi walilalamika kuwa upandishaji wa madaraja hufanywa na
mamlaka kama fadhila badala ya haki stahili ya mwalimu kulingana na sifa njema
alizo nazo. Waalimu walilalamikia zaidi urasimu mwingi uliopo katika
kupandishwa daraja, na vigezo vinavyotumiwa kumpandisha mwalimu daraja havikuwa
wazi, jambo linalofanya mchakato mzima kuwa na walakini. Mathalani, waalimu
walilalamika kuwa ili waweze kufikiriwa kupandishwa daraja, inawapasa ‘kuwa wema
na kuwa karibu’ na maofisa wa Idara ya Huduma kwa Walimu (TSD), chombo
kinachoshughulikia masuala ya kitaaluma ya waalimu, ikiwa ni pamoja na
upandishaji wa madaraja.
Pia, waalimu walilalamikia kuwepo kwa upungufu wa
nyumba, hali iliyowalazimu kuishi maisha duni sana kwani hawakuweza kumudu
gharama za makazi mazuri mijini kwa sababu ya mishahara duni waliyoipata.
Tatizo la makazi duni lilikuwa kubwa zaidi kwa shule za vijijini, hususan shule
za kata za serikali. Shule nyingi za kata za serikali zilizotafitiwa hazikuwa
na huduma ya umeme na hii ilifanya maisha ya waalimu kuwa duni zaidi. Hapa
chini kuna nukuu za maoni ya baadhi ya waalimu zinazothibitisha hali hiyo:
...Kama unavyoona shule yetu iko kilometa 20 kutoka
mjini. Hakuna umeme hapa, hakuna nyumba za waalimu. Tunatakiwa kupanga nyumba
kwa wenyeji, lakini nyumba zenyewe umeziona? Hivi, serikali hii inatufikiriaje?
Hivi hawajui kuwa na sisi ni binadamu, tumesoma na tunataka maisha mazuri? Na
mimi ninapenda kuona Manchester wakicheza, lakini ona: niko hapa, hakuna umeme,
hakuna usafiri kwenda mjini, na unataka nifundishe kwa furaha? (Mwalimu, Shule C, Mkoa wa Singida.)
Ni bahati mbaya tu kuwa mwalimu katika nchi hii.
Unapokea mshahara mdogo sana, na mshahara huohuo unakatwa vibaya mno, makato
mengi mno, ehee. Kwa mfano, kwa nini mchango wangu wa bima ya afya uongezeke
pale mshahara wangu unapoongezeka? Kwa nini wasiendelee na kiwango kilekile,
ukizingatia kwamba hata huwa siumwi kila siku? Kwa nini inakuwa hivi kwa
waalimu? (Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara.)
Ufundishaji duni na vifaa/zana duni za kufundishia
ilikuwa ni sababu nyingine iliyotajwa mara kwa mara ya wanafunzi kufanya vibaya
kitaaluma. Waalimu walilalamika kuwa shule zao kwa jumla hazikuwa katika hali
nzuri ya kuwezesha ufundishaji na ujifunzaji kufanyika. Mitazamo ya waalimu
katika eneo hili kwa kiasi kikubwa ilithibitisha matokeo ya utafiti uliofanywa
kwa njia ya hojaji na miongozo ya taarifa za shule. Mathalani, shule nyingi
hazina maabara na maktaba zinazofaa. Kadhalika, masomo mengi hayakuwa na vitabu
vya kutosha vya kiada na ziada. Kwa sababu hiyo, ufundishaji uliachwa ufanywe
kwa kutegemea juhudi za mwalimu mwenyewe, na hili halingewezekana ukitilia
maanani kiwango cha chini cha hamasa na moyo wa kujitolea kilichopo katika kazi
ya ualimu. Kwa mfano, waalimu walikuwa na maoni kama:
Shule zimekuwa mahali pa vijana kukulia, hakuna
ujifunzaji unaofanyika. Hakuna maktaba hapa, hakuna maabara, hakuna vitabu.
Waalimu wamechoka na wana huzuni wakati wote. Sasa utaiita hii shule, hee?
(Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida.)
Hata hivyo, licha ya kukosolewa sana kwa hali duni ya
mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, kulikuwa vilevile na maoni chanya
katika shule chache, hususan shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kikristo.
Katika shule hizi, hali ya zana za kufundishia na kujifunzia, kama
ilivyoonyeshwa katika matokeo ya utafiti kwa njia ya hojaji, ilikuwa nzuri mno
na yenye kutia moyo kuliko katika shule nyinginezo. Kwa sababu hiyo, waalimu wa
shule hizi waliamini kuwa shule zao zilikuwa zikifanya vizuri zaidi katika
mitihani kwa sababu zilikuwa na mazingira yanayofaa na yenye kurahisisha
mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji. Kwa mfano, mwalimu mmoja, ambaye
aliungwa na mkono kwa kauli moja na wengine katika kipindi cha majadiliano ya
vikundi lengwa, aliyetoka katika shule moja ya binafsi ya Kikristo mkoani
Singida, alikuwa na maoni haya:
Kwa jumla matokeo katika shule yetu ni mazuri. Hii ni kwa sababu shule ina zana bora za kufundishia
na kujifunzia, zikiwemo maabara. Vilevile tuna maktaba nzuri sana. Vilevile
waalimu wanahudhuria mara kwa mara programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga
kuboresha ufundishaji wao na kubadilishana mawazo na ujuzi, ambazo huandaliwa
na Tume ya Huduma za Jamii ya Kikristo.
Jambo jingine lililotajwa kusababisha wanafunzi
kufanya vibaya kitaaluma lilikuwa ni uongozi na usimamizi mbaya wa shule.
Walimu walio wengi katika shule nyingi zilizotafitiwa walikosoa uongozi wa
shule zao, wakidai kuwa haukuwa makini na mahitaji ya waalimu. Waalimu pia
walitoa maoni kwamba kulikuwa na mawasiliano duni kati ya waalimu na uongozi wa
shule zao. Wakikosoa zaidi, waalimu walitoa maoni kwamba hapakuwa na utaratibu
wa kutathmini kazi za waalimu hata pale walipofanya kazi kwa uwezo wao wote
katika mazingira magumu sana, badala yake uongozi wa shule ulikuwa mwepesi
kuwalaumu waalimu pindi wanafunzi walipofanya vibaya katika mitihani. Hapa
chini kuna nukuu za maoni ya baadhi ya waalimu kuhusu uongozi wa shule zao:
Uongozi wetu ni tatizo kubwa. Kwa mkuu wetu wa shule,
maendeleo ya taaluma ni suala lisilo muhimu sana. Hajali kama kuna zana za
kufundishia au la. Halafu, kuna mawasiliano duni sana kati yetu (waalimu) na
yeye: ni vigumu sana kumwona, hakuna mikutano. Anajifanyia kila kitu yeye
mwenyewe (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida).
Uongozi wetu wa shule hauko makini katika
kushughulikia matatizo ya waalimu. Hakuna usimamizi wa shughuli za ufundishaji,
hakuna semina kwa waalimu, hakuna anayejali. Mwalimu anaweza kufundisha kwa
mwaka mzima bila kuwa na andalio la somo, na hakuna atakayekuuliza. Shule haina
mwenyewe! (Mwalimu, Shule A, Mkoa wa Singida.)
Msingi duni wa wanafunzi kitaaluma na kitabia ni jambo
jingine lililotajwa kusababisha wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma. Hali hii
ilihusishwa zaidi na ukosefu wa maarifa ya msingi yanayohitajika ili kumudu
elimu ya sekondari. Waalimu walitoa maoni kwamba wanafunzi wengi wanaojiunga na
elimu ya sekondari, hususan shule za kata za serikali, wana msingi duni sana wa
kitaaluma kiasi kwamba hawawezi kumudu matakwa ya elimu ya sekondari. Kwa mfano,
waalimu walitoa maoni kwamba kiwango cha ujuzi wa kusoma na kuandika cha
wanafunzi wengi kilikuwa cha chini sana huku baadhi ya wanafunzi wakiwa hawajui
kusoma na kuandika. Zaidi ya hayo, baadhi ya wanafunzi walikuwa na ufahamu
mdogo sana wa lugha ya Kiswahili. Ni dhahiri kwamba hili ni tatizo kubwa kwa
sababu ikiwa wanafunzi hawawezi kuwasiliana kwa ufasaha kwa Kiswahili pindi
wanapojiunga na elimu ya sekondari, watatarajiwa vipi waweze kumudu masomo yao
ya sekondari yanayofundishwa kwa lugha ya Kiingereza? Hapa chini kuna nukuu za
maoni ya baadhi ya waalimu zinazothibitisha hali hii:
...kuna wanafunzi wengi wasiojua kusoma na kuandika
katika shule yetu. Ninafundisha kidato cha kwanza, na ninafahamu karibu
wanafunzi kumi ambao hawajui kusoma wala kuandika. Sasa, unategemea mimi
nitawasaidiaje? (Mwalimu, Shule U, Mkoa wa Mtwara.)
Hii ni shule ya kata (ya serikali). Tunapokea
wanafunzi duni sana, na kwa kweli tunapokea makombo: wale ambao hawakuweza
kuchaguliwa na shule za kitaifa za serikali. Wengi wa wanafunzi tunaowapokea
hawawezi kuandika vizuri, ujuzi wao wa Kiingereza ni mdogo sana na wanahitaji
muda mwingi ili waweze kumudu elimu ya sekondari (Mwalimu, Shule D, Mkoa wa
Singida).
4. Muhtasari, Hitimisho na Mapendekezo
Kwa kutumia mikabala yote miwili, mkabala wa kiidadi
na mkabala wa kiubora, utafiti huu umechunguza jinsi sifa za waalimu kitaaluma,
hamasa na moyo wa kujitolea walio nao katika kufundisha vinavyoathiri ufaulu wa
wanafunzi kitaaluma katika elimu ya sekondari. Utafiti huu ulifanywa katika
mikoa sita (6) katika shule 36, ukishirikisha waalimu zaidi ya 300 kutoka shule
za sekondari za serikali na za binafsi. Waalimu walishiriki katika utafiti huu
kwa kujaza hojaji na kupitia majadiliano ya vikundi lengwa.
Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwepo kwa masuala
kadhaa yanayohusiana na sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kujitolea
kufundisha walio nao waalimu na jinsi masuala hayo yanavyoathiri ufaulu wa
wanafunzi kitaaluma. Masuala hayo yanajumuisha haya yafuatayo:
i) Sifa za waalimu kitaaluma, hamasa na moyo wa kujitolea walio nao katika
kufundisha ni vigezo muhimu mno vinavyoukilia ufaulu wa wanafunzi kitaaluma.
Mwalimu kuwa na sifa nzuri za kitaaluma pekee bila moyo wa kujitolea
hakusababishi kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi kitaaluma kuimarika.
ii) Shule zenye waalimu wenye moyo wa kujitolea wa hali ya juu bila kujali
iwapo walikuwa na sifa za juu kitaaluma (shahada au zaidi) au la zilifanya
vizuri katika mitihani ya taifa. Kwa upande mwingine, shule zenye waalimu wenye
sifa za juu kitaaluma lakini wenye kiwango kidogo cha moyo wa kujitolea katika
kazi ya ualimu si lazima kwamba zilifanya vizuri katika mitihani ya taifa
kuliko zile zenye waalimu wenye sifa za wastani kitaaluma (stashahada au
chini). Hivyo, kwa mfano, shule za serikali zenye idadi kubwa zaidi ya waalimu
wenye sifa za juu kitaaluma hazikufanya vizuri kama shule binafsi za Kikristo
zenye idadi ya chini kiasi ya waalimu wenye sifa za juu kitaaluma.
iii) Mazingira mazuri ya kazi ndicho kigezo muhimu zaidi kinachoukilia
kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu katika kufundisha, na matokeo
yake kigezo hiki huwa na nguvu sana katika kuleta matokeo mazuri ya wanafunzi
kitaaluma. Matokeo ya utafiti huu yanazidi kuonyesha kuwa waalimu wa shule
binafsi za Kikristo wameridhika kwa kiasi kikubwa mno na mazingira ya kazi ya
shule zao kuliko waalimu wa shule za serikali na shule binafsi zinazomilikiwa
na watu binafsi. Hali hii, kwa kiasi fulani, huonyesha kwa nini wanafunzi wa
shule binafsi za Kikristo hufaulu vizuri mno kitaaluma kuliko wale wa shule za
serikali na shule nyingine za watu binafsi.
iv) Waalimu walio wengi katika shule za serikali, shule za Kiislamu na shule
za watu binafsi waliona kuwa uongozi wa shule zao ulifanya kazi kwa ufanisi mdogo
sana. Zaidi ya hayo, waalimu walioona kuwa uongozi wa shule zao ulifanya kazi
kwa ufanisi mkubwa walielekea kuwa na moyo wa kujitolea zaidi katika kazi ya
ualimu, na matokeo yake shule zao zilifanya vizuri zaidi katika mitihani ya
taifa kuliko shule ambazo waalimu wake waliona kuwa uongozi wa shule haukufanya
kazi kwa ufanisi.
v) Matokeo ya uchunguzi wa majadiliano ya vikundi lengwa (matokeo ya
kiubora) yanaonyesha kuwa kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu kwa
kazi ya ualimu ni cha chini kupindukia. Hali hii hujitokeza zaidi kwa waalimu
wa shule za serikali na shule za watu binafsi. Matokeo haya yanaonyesha kuwa,
kwanza, waalimu wachache tu ndio waliochagua kwa hiari yao kufanya kazi ya
ualimu na kwamba mazingira duni ya kazi yaliyopo katika shule nyingi za
serikali na mishahara midogo wanayoipata husaidia tu kuonyesha na kusisitiza
jinsi waalimu hao wasivyoipenda kazi ya ualimu. Athari za kiwango kidogo cha
moyo wa kujitolea walio nao waalimu ni kubwa mno na zinaonekana bayana kwa
kuwepo matokeo mabaya ya wanafunzi kitaaluma katika shule za serikali na za
watu binafsi. Zaidi ya hayo, kiwango kidogo cha moyo wa kujitolea walio nao
waalimu kwa kazi ya ualimu kwa kiasi fulani kinaweza kuonyesha msuguano mkubwa
uliopo miongoni mwa waalimu.
vi) Matokeo ya utafiti huu hayaonyeshi jinsi hali ilivyo katika shule zote
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu. Mathalani, wakati kiwango cha moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kilikuwa na uhusiano mkubwa na ufaulu wa wanafunzi
katika shule za serikali na shule za Kikristo, hapakuwa na uhusiano wa moja kwa
moja kati ya kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu na ufaulu wa
wanafunzi miongoni mwa shule zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu. Hali hii
inaonyeshwa na ukweli kwamba, wakati kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao
waalimu katika shule hizi kilikuwa cha juu kwelikweli, ufaulu wa wanafunzi
kitaaluma katika shule hizi ulikuwa duni kwelikweli. Hata hivyo, matokeo haya
hayana budi kutafsiriwa kwa uangalifu kwani ukubwa wa sampuli ya waalimu katika
shule za Kiislamu kwa kiasi fulani ilikuwa ndogo mno kulinganisha na shule
nyingine.
vii) Utafiti huu haukuchunguza kwa kina suala la vigezo vinavyotumiwa katika
kuwapangia waalimu masomo ya kufundisha, suala ambalo lilikuwa mojawapo ya
malengo ya utafiti huu. Sababu kubwa ni kwamba ilidhihirika kwamba hakika
waalimu hufundisha masomo waliyosomea katika vyuo vya ualimu au vyuo vikuu.
Hivyo, kigezo kikuu kilichotumiwa na wakuu wa shule kuwapangia waalimu masomo
ya kufundisha ni kwamba mwalimu anatakiwa kuwa amesoma somo hilo chuoni.
4.2 Hitimisho na Mapendekezo
Utafiti huu umeonesha mambo makuu matatu kuhusiana na
waalimu ambayo huchangia/kuamua ufaulu wa wanafunzi kitaaluma, nayo ni sifa za
walimu kitaaluma, kujituma na moyo wao wa kujitolea kwa kazi ya ualimu na
mtazamo walio nao kuhusu ufanisi wa uongozi wa shule. Pindi waalimu wanapokuwa
na moyo wa kujitolea na mtazamo chanya kuhusu uongozi wa shule, wanafunzi
huelekea kufanya vizuri zaidi katika kazi zao za kitaaluma.
Hata hivyo, ukiacha shule binafsi zinazomilikiwa na
asasi za Kikristo, matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa kiwango cha moyo wa
kujitolea walio nao waalimu kwa kazi ya ualimu ni cha chini sana na kwamba
waalimu walio wengi wanaona uongozi wa shule zao kuwa ni duni na usiofanya kazi
kwa ufanisi. Kiwango duni cha moyo wa kujitolea walio nao waalimu na uongozi
mbaya wa shule kwa kiasi fulani husababisha wanafunzi wa shule nyingi nchini
kufanya vibaya kitaaluma.
Kwa kuzingatia hitimisho hili, mapendekezo yafuatayo
yanatolewa kwa lengo la kuboresha kiwango cha moyo wa kujitolea walio nao
waalimu kwa kazi ya ualimu, na vilevile ufanisi wa uongozi wa shule, ambapo
matokeo yake kufanya hivyo kunaweza kuleta manufaa katika ufaulu wa wanafunzi
kitaaluma na kubadilisha hali duni ya matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato
cha nne. Mapendekezo haya yamefikiwa kutokana na matatizo yanayojitokeza katika
matokeo hayo, na vilevile kutokana na maoni ya washiriki kuhusu namna ya
kuboresha kiwango cha elimu nchini.
i) Kujituma na moyo wa kufanyakazi walio nao waalimu umejitokeza kama
tatizo kuu linaloathiri ufaulu wa wanafunzi kitaaluma, huku waalimu walio
wengi, hususan katika shule za serikali, wakionyesha kuwa na kiwango cha chini
sana cha moyo wa kujitolea kwa kazi ya ualimu. Kiwango hiki kidogo sana cha
moyo wa kujitolea walio nao waalimu kinasababishwa zaidi na malipo duni na
mazingira duni ya kazi katika shule na kile ambacho waalimu wanakiita ‘serikali
kutojali’ kazi ya ualimu. Ili kuinua moyo wa kujitolea wa waalimu kwa kazi ya
ualimu, hatua zifuatazo hazina budi kutiliwa maanani:
a. Serikali na wadau wengine wanapaswa kushughulikia kwa dhati tatizo la
mazingira duni ya kazi wanayokabiliana nayo waalimu, ikiwa ni pamoja na tatizo
la makazi, huduma za jamii kama vile maji na umeme.
b. Suala la malipo duni lilijitokeza kama tatizo kubwa katika kuvutia
waalimu kujiunga na kuendelea na kazi ya ualimu. Mishahara ya waalimu bado ni midogo mno kiasi cha kusikitisha. Ikumbukwe
kwamba utafiti huu na tafiti nyingine nyingi zimeonyesha kila mara kwamba
malipo duni ndiyo sababu inayowakatisha tamaa sana waalimu. Hivyo basi, tatizo
hili halina budi kushughulikiwa kama tatizo la dharura iwapo tunataka kuboresha
kiwango cha elimu na kubadilisha hali duni ya matokeo ya mitihani ya taifa.
Sambamba na kuboresha malipo ya waalimu, suala la kuwapandisha waalimu madaraja
kwa wakati halina budi kushughulikiwa kwa kupunguza urasimu usio wa lazima
katika mchakato huo. Kwa sasa waalimu wengi wamefanywa kuamini kuwa kupandishwa
daraja ni suala la wateule wachache, badala ya kuwa suala la stahili ya mwalimu
kulingana na sifa njema alizo nazo.
c. Tunapaswa kuwa na viwango vya chini kabisa vinavyokubalika vya shule
kuitwa shule. Kwa sasa, kuna tofauti kubwa sana miongoni mwa shule, kwani kuna
zile zinazohangaika hata kupata chaki na shule zenye vifaa vya kutosha
kama vile maktaba na maabara. Programu zetu za elimu ambazo zinaonesha kwa muda
mrefu mno zimekuwa zikijishughulisha zaidi na idadi hazina budi kupitiwa upya
na kutilia maanani zaidi suala la kuongeza ubora.
d. Ni muhimu kuwa na taratibu za kuwatambua na kuwatuza waalimu
wanaofanya kazi kwa kiwango kizuri sana kuzidi wengine. Kwa sasa, juhudi za
ziada za waalimu hazitambuliwi wala kutuzwa. Wakati wa majadiliano ya vikundi
lengwa, waalimu wengi walilalamika kwamba wanafunzi pekee ndio wanaotambuliwa
na kutuzwa pindi wanapofaulu vizuri sana. Lakini tunaelekea kusahau kwamba kwa
kila mwanafunzi anayefaulu vizuri sana, kuna mwalimu aliyefanya juhudi zaidi
kumwezesha kufaulu, na juhudi hizi hazina budi kutambuliwa na kutuzwa ipasavyo.
e. Ni suala muhimu sana kwenye kazi ya ualimu, walimu wenyewe
wakifahamu kikamilifu Sera ya Elimu na Mafunzo na maelekezo/maagizo mengine
yote na program/mipango inayotolewa na viongozi ngazi za juu kuletwa kwao.
Walimu kuzielewa sera na mipango ni muhimu sana ili wazitekeleze
vyema na kwa tija, hatimaye waboreshe ufanisi wa sekta ya elimu na
uwajibikaji
f. Mchakato wa kudahili wanafunzi wanaokwenda kujiunga na kozi ya ualimu
tarajali vyuoni kuna haja ya kuupitia upya na kuuboresha. Tanzania
inahitaji watu ambao si tu wana shauku ya kufundisha bali
wawe na nia thabiti na uwezo wa kufundisha kwa ufanisi. Vigezo vya
kudahili wanafunzi wanaokwenda kusomea ualimu na kufundisha vinapaswa kuwa
sawa kwa wale waliofaulu vizuri tu masomo yao ngazi za sekondari kama ilivyo
kwa wanaochukuliwa kusomea udaktari na sheria.Kushindwa kufanya hivyo tutaendelea kudhoofisha ubora
wa elimu na maendeleokatika nchi yetu.
g. Maadili kwa Walimu, kujituma uwajibikaji na uaminifu ni muhimu
sana katika kurejesha hadhi na thamani ya taaluma yao kwa
ujumla. Walimu wakumbuke kuwawamebeba jukumu kubwa la
maendeleo ya Tanzania na wana mchango wa kipekee kwenye kujenga
mustakabli na mwelekeo wa nchi yetu. Walimu wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa
kwenye jamii na kwenye taaluma yao.
h. Walimu kufahamu haki zao na kusubiri wengine kuzitetea
na kuzilinda hakutoshi, nilazima wajipange na kuchukua hatua kamili na za
uhakika bila kukata tamaa hadi watakapoona haki zao zimetekelezwa, huku
wakihakikisha wanawajibika kwa viwango kubalifu kwa jamii.
ii) Ili kuboresha utendaji kazi wa waalimu kitaaluma, kuna haja ya kufufua
programu endelevu za mafunzo kazini kwa waalimu. Kwa sasa, programu hizi ni
adimu, nazo hutolewa mara moja moja huku zikiwa na nguvu ndogo ya kuboresha
weledi wa waalimu. Hapana budi vilevile kuwa na programu za mara kwa mara za
mafunzo ya uongozi wa shule kwa sababu utafiti huu umeonesha kuwa waalimu wengi
katika shule nyingi wanasikitishwa sana na uongozi wa shule zao, jambo ambalo
hatimaye huathiri moyo wa kujitolea walio nao na hamasa yao ya kufundisha.
iii) Misingi duni ya kitaaluma ya wanafunzi ilijitokeza kama mojawapo ya
sababu kuu za kuongezeka kwa kiwango cha wanafunzi waliofeli katika Mtihani wa
Taifa wa Kidato cha Nne. Katika baadhi ya shule, hali ilishtua kwa kiasi fulani
kubaini kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari hawakujua kuandika!
Hivyo basi, kuna haja ya kuchunguza tena mwenendo wa Mtihani wa Darasa la Saba
na pengine kufikiria kuimarisha Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili kwa
kurejesha tena viwango vya kufaulu mtihani huo.
iv) Utafiti huu ulitumia sampuli ndogo tu ya shule zilizochaguliwa kwa
kufuata utaratibu maalumu badala ya kuzichagua kiholela. Hakika, baadhi ya
vipengele vya shule kama vile shule za Kiislamu viliwakilishwa vibaya kwani
idadi ndogo tu ya shule ndiyo iliyoshiriki. Kwa sababu hiyo, majumuisho kuhusu
matokeo haya hayana budi kufanywa kwa tahadhari na umakini sana.
v) Utafiti huu umechunguza kiwango cha kujituma na moyo wa kujitolea katika
kazi miongoni mwa waalimu. Ili kufanya ulinganifu, tafiti zitakazofuatia hazina
budi kulenga namna ya kupata kiwango cha kujituma, nia ya kufanya kazi na moyo
wa kujitolea miongoni mwa walimu na taaluma nyingine ili kuoanisha matokeo ya
utendaji kwa ujumla.
Marejeo
Caprara, G.V., Barbaranelli, C., Steca,
P. & Malone, P.S. (2006). Teachers’
self-efficacy beliefs as determinants of job satisfaction and students’
academic achievement: A study at the school level. Journal of School
Psychology, 44, 473-490.
Ministry of Education and Vocational
Training (MoEVT, June 2010). Secondary Education Development Programme II (July
2010-June 2015).
Mosha, H.J. (1988). A reassessment of
the indicators of primary education quality in developing countries: Emerging
evidence from Tanzania. International Review of Education, 17-45.
Mosha, H.J. (2011). The state of quality
of education in Tanzania: A candid reflection. Makala iliyowasilishwa katika Kongamano la Elimu, Dar
es Salaam (Juni 2011).
National Examinations Council of
Tanzania (NECTA, 2011). Examination results – Statistics for October 2010
results.
Oduro, G.K.T., Dachi, H., & Fertig,
M. (2008). Educational leadership
and quality education in disadvantaged communities in Ghana and Tanzania.
Makala iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa Baraza la Jumuiya ya Madola la Uongozi
na Usimamizi wa Elimu, Durban, Afrika Kusini (Septemba 2008).
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (wa 61,
Oktoba 2006). Wazungumzaji wanasisitiza umuhimu wa elimu katika kufikia malengo
ya maendeleo ya kijamii, Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Inapatikana katika
intaneti:http://www.un.org/News/Press/docs/2006/gashc3847.doc.htm
Uwezo (2010). Are our children
learning? Annual Learning Assessment Report Tanzania 2010. Dar es Salaam:
Uwezo, TENMET & Hivos/Twaweza.
[1] Shule
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu ziliondolewa katika uchambuzi huu kutokana
na idadi ndogo sana ya shule hizo katika sampuli hii. Shule moja tu ndiyo
iliyokuwa na sifa za kujumuishwa katika uchambuzi wa mwisho.
[2] Shule
zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu ziliondolewa katika uchambuzi huu kutokana
na idadi ndogo sana ya shule hizo katika sampuli hii. Shule moja tu ndiyo
iliyokuwa na sifa za kujumuishwa katika uchambuzi wa mwisho.
[4] Kwa
mara nyingine, ikumbukwe kwamba waalimu 11 tu kutoka shule moja tu ndio
waliounda sampuli ya shule binafsi zinazomilikiwa na asasi za Kiislamu.
[5] Data
kuhusu waalimu wa shule za Kiislamu hazina budi kuchambuliwa kwa uangalifu kwani
sampuli yao iliundwa na washiriki wachache tu.
Labels: HABARI
0 Comments:
Post a Comment
Subscribe to Post Comments [Atom]
<< Home