Tuesday, 1 April 2025

MUHTASARI WA KIKAO CHA WANA UKOO KILICHOFANYIKA TAREHE 26/02/2025 KATIKA MSIBA WA MZEE METHUSELA KAJANA MARINGO. WAJUMBE: Kikao kilihudhuriwa na Wajumbe wapatao 50. Kilisimamiwa na Malembo Aman aliyekuwa M/kiti, Dishon Maringo aliyekuwa Katibu na Seleman Kajana aliyekuwa mweka kumbukumbu wa Kikao (Mwandishi). AGENDA: 1. KUFUNGUA KIKAO Kikao kilifunguliwa na M/kiti wa kikao ndugu Malembo Aman mnamo saa 3:00 usiku. M/kiti aliwashukuru wajumbe kwa kutoa muda wao na kuhudhuria kikao. Kabla ya kuanza kikao, ombi la kukiweka kikao uweponi mwa Bwana lililetwa na mmoja wa wajumbe wa kikao. 2. KERO MBALIMBALI ZINAZO ZOROTESHA MAENDELEO YA UKOO Baada ya kufunguliwa kwa kikao, wajumbe waliweza kuibua mambo kadha wa kadha ambayo yalionekana kama kero zinazoweza kuharibu ustawi wa Ukoo kama ifuatavyo: a) Kutokuwepo kwa vikao vya mara kwa mara vya ukoo Matatizo na migogoro mbalimbali ndani ya ukoo yamesababishwa na kutokuwepo kwa vikao vya mara kwa mara katika ukoo. Kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa vikao hivi, wajumbe kupitia kikao hiki, wameazimia kuwepo kwa Kikao cha ukoo kitakachokuwa kinafanyika mara moja kwa mwaka kila ifikapo tarehe 30 ya mwezi Julai. Kwa mantiki hii kikao cha kwanza kilipangwa kufanyika Tarehe 30/7/2026. Wajumbe wote waliridhia kuwa vikao vyote vitakuwa vikifanyika Katika Kijiji cha BUSAMBARA ambako ndiko liliko chimbuko la waasisi wa Ukoo wetu. Hivyo kila mjumbe atakayehudhuria kikao hicho anapaswa kutoa kiasi cha shilingi 10,000/= za Kitanzania kama gharama ya uendeshaji wa shughuli nzima za kikao. Na mchango unapaswa kuwasilishwa mwezi mmoja kabla ya Tarehe ya kikao. b) Hoja ya kulima hadi kwenye makaburi Iliibuliwa hoja kuwa kuna wana ukoo wanaolima ardhi iliyoachwa na waasisi wetu kulima hadi kwenye makaburi yaliyohifadhi miili ya wapendwa wetu waliotangulia mbele za haki. Kikao kupitia wajumbe wake kiliazimia kuwa, wanaolima ardhi hiyo waache walau Mita tatu (3) kuzunguka pande zote za eneo la Makaburi ili kuondoa kero ya kulima hadi kwenye Makaburi. c) Mustakabari wa utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi ya ukoo Kumekuwepo kwa migogoro kuhusu ardhi iliyoachwa na waasisi wetu wa ukoo. Hii imepelekea baadhi ya wana ukoo kutosalimiana hadi kufikia hatua ya kushikana uchawi kwa sababu ya mashamba haya ya ukoo. Kuhusiana na mgogoro huu kikao kiliazimia kufanya yafuatayo:  Ardhi hii igawanywe upya katika sehemu mbili ambazo ni Uzao wa Maingu Maringo na Kajana Maringo na mipaka iwekwe upya.  Kila uzao uangalie namna nzuri ya kuweza kutumia ardhi hii bila kusababisha migogoro yoyote na sehemu moja ya Uzao isiingalie ardhi isiyowahusu isipokuwa kwa makubaliano maalumu.  Ukoo uangalie nmna ya kusajili ardhi ya ukoo huu ili umiliki wake utambulike kwa nyaraka za kiserkali. Hii itasaidia kuondoa migogoro kati ya Ukoo na Serikali pale Serikali itakapokuwa na maamuzi mengine ya matumizi ya ardhi hii ya ukoo. d) Hoja ya wana ukoo kutotambuana Katika kikao hiki ilibainika kuwa wana ukoo wengi hawafahamiani. Hivyo kwa kutumia Siku ya kuanua Matanga yaani Tarehe 27/02/2025 kikao kiliazimia ufanyike utambulisho wa kipekee ili wana ukoo wote waweze kufahamiana kwa kina. e) Hoja ya kuwepo kwa utovu wa nidhamu (Indiscipline cases) Kikao kilibaini kuwepo kwa watoto wenye nidhamu mbaya ndani ya ukoo. Na katika uchunguzi wa awali, kikao kilibaini utovu huo wa nidhamu miongoni mwa watoto, unasababishwa na malezi wanayokutana nayo ndani ya familia zao. Hivyo kikao kilitoa rai kwa wazazi wao kutoa malezi yenye maadili yatakayowasaidia watoto wao kuwa na nidhamu ndani na nje ya ukoo. 3. MENGINEYO a. Katika kipengele hiki cha mengineyo, mjumbe (Dishon Maringo) alibainisha kero yake ambayo iliwalenga moja kwa moja dada zake na wadogo zake wa kike kutowapa ushirikiano Mawifi zao na kuwasubiri waharibu ili wawaseme. Akiwasilisha hoja hiyo, mtoa hoja alibainisha kuwa dada hawa wanatakiwa kuwa marafiki kwa Mawifi zao ili kuwaelekeza wanayotakiwa kufanya katika matukio makubwa kama haya. Ili kuondoa kadhia hii kikao kiliazimia tabia hiyo kukomeshwa mara moja ili kujenga uhusiano wenye afya. b. Kuhusu wana ukoo wasiotoa michango kwenye matukio ya misiba. Kwa wale waliobainika kutotoa michango kwenye daftari la ukoo, waliombwa kuwasilisha michango hiyo haraka iwezekanavyo. 4. UCHAGUZI WA VIONGOZI WA VIKAO VYA UKOO Kupitia kikao hiki, wajumbe walipata fursa ya kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi watakao kuwa wakisimamia na kuratibu shughuli zote za vikao vya ukoo kama ifuatavyo: M/Kiti wa Vikao vya Ukoo atakuwa ni: BIGAMBO AMAN Katibu wa Vikao vya Ukoo atakuwa ni: DISHON K. MARINGO Mhazini wa Vikao vya Ukoo atakuwa ni: JUDITH K. MARINGO 5. KUFUNGA KIKAO Baada ya kikao kufanyika kwa masaa manne na nusu, Mwenyekiti ndugu Malembo Aman aliwashukuru wajumbe kwa uvumilivu wao kisha akatamatisha shughuli zote za kikao hicho majira ya saa Saba 7:20 usiku na kutoa nafasi kwa wajumbe kwenda kupumzika. Muhtasari huu wa kikao umeandaliwa na ndugu Seleman Melijo Kajana Aliyekuwa Mweka kumbukumbu za Kikao (Mwandishi)